FIFA, TFF waanza utambuzi wa vipaji Rukwa.
Na Israel Mwaisaka, Nkasi.
Zoezi la utambuzi wa vipaji vya soka kwa watoto wa kike na kiume wenye umri wa miaka 12-16 limeanza mkoani Rukwa, likilenga kuandaa wachezaji wa baadaye wa timu za taifa.
Zoezi hilo linaendeshwa chini ya wataalam kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), ambapo mchakato wa awali wa ulianza rasmi ngazi ya halmashauri katika wilaya nne za mkoa wa Rukwa kuanzia Machi 12, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa zoezi hilo, Mkuu wa Idara ya Utambuzi wa Vipaji kutoka TFF, Gidion Ngereza, alisema kuwa jumla ya watoto 180 walichaguliwa kuendelea kwenye hatua ya mkoa, iliyoanza Machi 16, 2026 na kuendelea kwa siku tano mkoani humo.
Ngereza alisema kuwa lengo kuu la zoezi hili ni kutafuta wachezaji wa kike na kiume wenye vipaji ambao wanaweza kuingia kwenye timu ya taifa ya vijana.
Aliongeza kuwa zoezi hili linafanyika katika mikoa 32 na halmashauri 184 kote nchini.
Aidha, Ngereza aliwahimiza wazazi na walezi kuunga mkono watoto wao kushiriki kwenye zoezi hilo, kwani itawasaidia kupata ujuzi, uzoefu, na fursa za kujiri kupitia sekta ya michezo.
Alibainisha kuwa programu hiyo ni miongoni mwa mikakati ya TFF na FIFA wa kuimarisha michezo kwa vijana nchini Tanzania na kwamba watoto bora watapatiwa mwongozo na mafunzo ya kitaalamu ili kuwa wachezaji wa viwango vya juu.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania limeahidi kuendeleza zoezi hili kwa kuunganisha rasilimali na ushauri wa wataalamu kutoka FIFA, huku likihakikisha kuwa hakuna mtoto anayepoteza fursa kutokana na changamoto za kifedha au kijiografia.



Comments
Post a Comment