Watumishi wawili halmashauri ya Nkasi wafukuzwa kazi kwa utovu wa nidhamu
Na Israel Mwaisaka, Nkasi
Baraza la madiwani Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa, limewachukulia hatua za kinidhamu watumishi wawili wa kada ya Afya kwa kuwafukuza kazi kwasababu ya utoro wa muda mrefu katika vituo vyao vya kazi
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Mashauri ya kinidhamu kilichoketiwa na madiwani hao, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Richard Leonard Masai alisema wamejiridhisha na taarifa za watumishi hao za kuwa watoro wa muda mrefu katika maeneo yao yakazi, hivyo wanakila sababu ya kuwafukuza kazi ili iwe fundisho kwa wengine.
Watumishi waliofukuzwa kazi ni Lyangawe Charles Lutu muuguzi daraja la II kituo cha afya Kirando na Gaudensia Fredrick Lukago muuguzi msaidizi daraja II kituo cha afya Kabwe.
Pia Baraza hilo la madiwani , jana limepitisha mapendekezo ya rasimu ya mpango na bajeti ya Halmashauri hiyo kwa Mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo Halmashauri inakadiria kukusanyana na kutumia jumla ya shilingi billion 47.3.
Akiwasilisha mapendekezo ya rasimu ya mpango na bajeti Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo Steward Vidoga, alisema mapendekezo ya bajeti yamelenga kutekeleza shughuli mbalimbali za Kutoa huduma za jamii, kuboresha miundombinu na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa asilimia 100 ya makisio ya mwaka 2026/2027.
Aidha kupitia baraza hilo waheshimiwa madiwani, wamejadili mapitio ya mpango na bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2025/2026, kuanzia Julai hadi Disemba, ambapo wamempongeza Mkurugenzi Mtendaji Afraha N. Hassan kwa kusimamia mapato na shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kipindi ambacho hakukuwa na Baraza la madiwani.





Comments
Post a Comment