MWANAMKE AUAWA KWA RADI AKITOKA SHAMBANI
Na Israel Mwaisaka,Nkasi
Mwanamke aliyefahamika kwa jina la Magreth Chakupewa (26) mkazi wa kijiji Cha Kate kata ya Kate wilayani Nkasi amefariki Dunia baada ya kupigwa na radi.
Shuhuda wa tukio hilo Crisence Kwimba amesema kuwa tukio hilo limetokea leo jumamosi majira ya saa 11 jioni wakati Mwanamke huyo alipokuwa ametoka shambani.
Amesema kuwa marehemu kabla ya mauti kumkuta alikua ametoka shambani huku akiwa ameambatana na mwenzie na baada ya muda radi ilitua na kumpata Mwanamke huyo na kupoteza maisha huku mwenzie akisalimika na kukimbilia kijijini kwenda Kutoa taarifa juu ya tukio hilo.
Baba wa marehemu Joseph Chakupewa amedai kuwa mtoto wake huyo alitoka asubuhi kuelekea shambani anakojishughulisha na kilimo Cha Mahindi lakini jioni alishitushwa na taarifa za kifo hicho kilichotokana na radi.
Amedai kuwa mtoto wake huyo Hadi mauti yanamkuta ameacha mtoto mdogo wa kike wa mwaka mmoja na miezi 7
Afisa mtendaji wa kata ya Kate Victor Chang'a amekiri kutokea kwa changamoto hiyo na kuwa taratibu zote za kiserikali zimefanyika na kujiridhisha kuwa kifo hicho kimetokana na radi.
Amesema kuwa eneo hilo la Kate limekuwa na matukio ya mara kwa mara ya radi na kuwa ipo haja ya elimu kutolewa juu ya kukabiliana na matukio hayo ya mara kwa mara.
Mkuu wa wilaya Nkasi Peter Lijualikali amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka Wananchi kuendelea kuchukua tahadhari katika kipindi hiki Cha mvua kwa kufuata maelekezo ya wataalamu namna ya kujikinga na majanga mbalimbali ikiwemo ya radi.

Comments
Post a Comment