MWAKATENYA:Bodaboda zingatieni sheria na kuongeza ujuzi kwa kwenda vyuo vya udereva
Na Israel Mwaisaka, Nkasi
Balozi wa kudhibiti na kupambana na uvuvi haramu ukanda wa maziwa makuu Pascal Mwakatenya amewataka Maafisa usafirishaji (Bodaboda) watengeneze mazingira ya kujiheshimu na kuheshimu kazi Yao kwani kwa kufanyia hivyo kutapelekea jamii iwaheshimu na kufanyia kazi hiyo katika mazingira mazuri.
Hayo ameyasema Jana alipokuwa akizungumza na Bodaboda wa stendi kuu Namanyere wilayani Nkasi kwenye sherehe za kuukaribisha mwaka mpya wa 2026 zilizoandaliwa na Bodaboda hao kama sehemu ya mkakati wa kuanza kazi hiyo katika msimu wa mwaka huu wa 2026.
Amesema kuwa Bodaboda ni kazi kama ilivyo kazi nyingine hivyo ni jukumu lao kuhakikisha heshima ya kazi Yao inajengwa na wao wenyewe kufanya kazi hiyo kwa weredi ikiwa ni pamoja na kujiepusha na matendo yoyote maovu ili waweze kuheshimika na jamii.
Balozi Mwakatenya amewasisitiza waendelee kufuata sheria za usalama barabarani kwani hiyo ndiyo itakua njia pekee ya kuepuka misukosuko isiyokuwa ya lazima ya kukamatwa na hata kutozwa faini badala ya muda huo kuutumia kujijenga kimaisha na kuweza kutunza vyema familia zao.
Pia aliwataka Bodaboda hao kukua na kwenda mbele zaidi kuendesha magari badala ya kudumaa kwenye kazi hiyo ya Bodaboda ikiwa ni pamoja na kujihusisha na shughuli nyingine za ujasiliamali badala ya kuitegemea kazi hiyo pekee kwa ustawi wa maisha Yao
Awali Bodaboda hao katika risala yao walimweleza mgeni rasmi kuwa changamoto kubwa waliyonayo ni ya mikataba kandamizi kati Yao na wamiliki wa pikipiki na kuomba uwepo wa mikopo rafiki ikiwa ni pamoja na kutokuwa na bima.
Waliomba Serikali kuingilia kati juu ya mikataba hiyo kandamizi kati Yao na wamiliki wa pikipiki hizo na kuwa wanajikuta muda mwingi wakiutumia kumtumikia mmliki wa pikipiki na wao kuendelea kuwa masikini licha ya kufanya kazi hiyo kwa nguvu zote.
Kufuatia maombi hayo Mwakatenya aliomba suala la mikopo alibebe na kulipeleka kwenye mamlaka husika za Serikali lakini juu ya suala la bima alitoa fedha kiasi Cha Tshs,1000,000 ili zisaidie baadhi ya Bodaboda hao kulipia bima zao na kuwa ataendelea kuwasaidia hadi wote wawe na bima.

Comments
Post a Comment