WATUMISHI WA MAKAO MAKUU OFISI YA MKURUGENZI WAPATIWA ELIMU YA MAGONJWA YA AFYA YA AKILI.
Na Asha Hassan,Nkasi
Magonjwa ya afya ya akili ni miongoni mwa magonjwa yanayosababisha msongo wa mawazo kwa watumishi walio wengi, na kusababisha majukumu yao kutoyatekeleza vizuri.
Ili kuhakikisha tatizo hilo linadhibitiwa kwa Watumishi, Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa Leo Novemba 24,2025 kwakushirikiana na Mtaalamu wa afya ya akili wilayani humo wameandaa mafunzo kwa watumishi wa Halmashauri hiyo ili kukabiliana na tatizo hilo.
Akizungumza katika mafunzo hayo Mratibu wa Magonjwa yasiyoyakuambukiza (W) Nkasi Richard Kauzeni amesema kuwa lengo la mafunzo hayo kwa watumishi nikuwaelimisha ili waweze kujua changamoto na athari za msongo wa mawazo zinatokana na Nini na namna ya kukabiliana nazo mahala pa kazi.
Aidha ameongeza kuwa kwa sasa Watumishi wengi wanakabiliwa na tatizo hilo mahala pa kazi, hivyo mafunzo hayo yatawasaidia kutatua tatizo la msongo wa mawazo.
Sambamba na hayo ameeleza kuwa changamoto ya msongo wa mawazo kwa watumishi inapelekea kukosa morali ya kazi hivyo kuwa na utendaji mbovu wa kazi na taasisi kupata hasara lakini pia uzalishaji pamoja na utoaji huduma unakuwa sio rafiki au haukidhi matakwa ya wananchi na kusababisha Serikali kunyooshewa kidole.
Hata hivyo amesema yapo mambo kadhaa yanayopelekea kwa watumishi kupata msongo wa mawazo ikiwemo wengi wao kuwa na mahitaji makubwa ya kupata vitu vingi kwa wakati mmoja kupita vipato vyao.
Kwa upande wake kaimu Afisa Utumishi Emmanuel Shombe kupitia mafunzo hayo amewataka Watumishi kutotegemea mishahara pekee, badala yake wawe na vyanzo vingine vya mapato ili kuepukana na mikopo isiyoyalazima ambayo hupelekea msongo wa mawazo kwa watumishi.
Shombe amesema ili kuendelea kupeana elimu, zaidi kutakuwa na mwendelezo wa mafunzo ya aina hiyo pamoja na mafunzo ya matumizi sahihi ya pesa.
Nao baadhi ya watumishi walioshiriki mafunzo hayo Bw. Renatus Danda pamoja na Abdul Mtani wamesema mafunzo hayo yamewajenga kwa asilimia kubwa kwani wamepata uelewa mkubwa na watayafanyia kazi pamoja na kuwasaidia watu wengine.


Comments
Post a Comment