Watendaji kata na vijiji waaswa kusimamia amani
Na Israel Mwaisaka,Nkasi
Mkuu wa wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa Peter Lijualikali amewataka Maafisa watendaji kata na vijiji kuhakikisha wanasimamia suala Zima la amani katika maeneo yao ili wananchi waendelee kufanya kazi na kujiletea maendeleo.
Akizungumza kwenye kikao kilichowajumuisha watendaji hao na viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama wa wa wilaya kwenye ukumbi wa Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya November 28, 2025, amesema kuwa wao kama viongozi, moja ya jukumu lao kubwa ni kuhakikisha suala zima la amani na utulivu linakuwepo katika maeneo yao, ikiwa ni pamoja na kusimama miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika kata na vijiiji vyao.
Amedai kuwa hivi karibuni Waziri Mkuu Dk.Mwigulu Lameck Nchemba, alitoa agizo la Kila mtumishi wa Umma kuwajibika katika nafasi yake hivyo wao kama watendaji wanalo jukumu la kuhakikisha kuwajibikaji kwa watumishi wanaowaongoza unakuwepo.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya amewataka watendaji hao kuwatumia watu maarufu katika maeneo yao wakiwemo wazee na viongozi wa kimila, kuzungumza na kuyaonya makundi ya vijana kutojihusisha na suala Zima la uvunjifu wa amani kwani athari zake zinaathiri uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Ameongeza kuwa suala la usimamizi wa miradi ni jukumu la Kila Mtendaji wa kata na Kijiji na kudai kuwa endapo miradi itatekelezwa chini ya kiwango wao ndio watakuwa wakwanza kuwajibika kabla ya wahusika wengine wanaotekeleza mirada hiyo.
Sambamba na hayo amewaagiza watendaji hao kuhakikisha kuwa wanakuwa na daftari la orodha ya kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi, ili kuweza kuleta mahisiano mazuri baina ya wananchi na serikali, pamoja na kutoa huduma kulingana na mahitaji ya jamii.
Hata hivyo wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama, wamegusia suala la kuwepo kwa maandamano yasiyo rasmi, hivyo jukumu lao ni kuhakikisha halitokei, kwakuzungumza na wananchi kupitia mikutano na kuimarisha ulinzi katika maeneo yao ili watu wawe salama.


Comments
Post a Comment