Naibu katibu mkuu avutiwa na kasi ya Wakandarasi Wanawake-Songwe



Na Ibrahim Yassin, Songwe

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Dk. Charles Msonde, amepongeza kasi na ubora wa ujenzi wa barabara unaotekelezwa na wakandarasi wanawake wazawa mkoani Songwe, akisema wameanza vizuri na wanaonyesha uwezo mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya serikali.

Dk. Msonde alitoa pongezi hizo leo, Oktoba 15, 2025, wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja katika wilaya za Ileje na Mbozi.


Akiwa wilayani Ileje, alikagua Daraja la Sange, linalojengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 7.942, ambapo ujenzi unaendelea kwa kasi nzuri.
Baada ya kukagua, Dk. Msonde aliagiza wakandarasi kuongeza kasi ya ujenzi, ikiwemo kufanya kazi usiku na mchana ili miradi ikamilike kwa wakati.

Akizungumza katika ziara hiyo, Dk. Msonde alisema ameridhishwa na matumizi ya fedha za serikali, akibainisha kuwa fedha zimetumika ipasavyo na miradi inaonyesha tija kwa wananchi.


Katika wilaya ya Mbozi, alikagua ujenzi wa Barabara ya Ruanda–Nyimbili–Hasamba–Izyila–Itumba, yenye urefu wa kilomita 79.67 kwa kiwango cha lami, pamoja na sehemu za barabara ya Ruanda–Idiwili kuanzia kilomita 2 hadi 21.
Amesema barabara hizo ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kuharakisha maendeleo vijijini na kuimarisha miundombinu ya usafiri na uchumi.

> “Nimeridhishwa na kazi inayoendelea. Wakandarasi wanawake wameonyesha mfano bora wa ujenzi wa barabara zenye viwango. Serikali itaendelea kuwaunga mkono,” alisema Dk. Msonde.


Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wakandarasi Wanawake Tanzania (TAWOMA), Bi. Judith Odunga, alisema watahakikisha wanakamilisha miradi hiyo kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

> “Tunaomba serikali ituongezee fedha ili tuweze kuendana na kasi ya ujenzi wa barabara hizi muhimu,” alisema Bi. Odunga.

Dk. Msonde alimalizia kwa kusema serikali itaendelea kuwezesha wakandarasi wanawake ili kuongeza ushiriki wao katika miradi mikubwa ya ujenzi nchini, ambapo awali walipewa miradi ya Shilingi Bilioni 10, lakini sasa wanatarajiwa kufikia hadi Bilioni 50 kutokana na uwezo waliouonyesha.


Comments

Popular posts from this blog

KAEGELE NA KAZUKAMWE WAIBUKA KIDEDEA KURA ZA MAONI CCM WILAYANI NKASI

DIWANI KATA YA KALA AFARIKI DUNIA KWA UGONJWA WA KIHARUSI

Mke wa Mchungaji wa kanisa la EAGT ajinyonga akihofia deni lake la fedha za kanisa