Kampeni ya "Tuwaambie"kabla hawajaharibiwa yazidi kupamba moto
Na Ibrahim Yassin, Mbozi
Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi Wilaya ya Mbozi limeendelea na utekelezaji wa kampeni ya “Tuwaambie kabla hawajaharibiwa” awamu ya pili, kwa kutoa elimu kwa wanafunzi wa kidato cha nne na sita, katika Shule ya Sekondari Myovizi, iliyopo kata ya Mahenje wilaya ya Mbozi, mkoa wa Songwe.
Akitoa elimu hiyo, Sajenti wa Polisi Merina, alisema kampeni hiyo inalenga kuwalinda watoto wa kike na wa kiume wanaotarajia kuhitimu elimu ya sekondari na msingi, ili wanapokutana na changamoto za maisha ya mtaani waweze kujilinda na kuepuka hatari zinazoweza kuharibu ndoto zao.
Sajenti Merina aliwapa uelewa kwenye mada mbalimbali kama elimu ya ukatili wa kijinsia, namna ya kuripoti vitendo vya ukatili, aina za ukatili, maadili mema na uzalendo.
“Jamii imeanza kuharibika kutokana na vitendo vya ukatili na mmomonyoko wa maadili, hivyo ni wajibu wetu kuongeza jitihada kubwa kuwaelimisha watoto ambao ndiyo taifa la kesho,” alisema Sajenti Merina na kusisitiza kuwa vitendo vya ukatili havina nafasi katika jamii.
Kwa upande wao, Walimu wa Shule ya Sekondari Myovizi, Wamepongeza Dawati la Jinsia na Watoto kwa kutoa elimu hiyo muhimu wakisema kuwa elimu hiyo itawajenga wanafunzi kujitambua na kuwa na msimamo imara wanapokabiliana na changamoto za maisha.
Nao baadhi ya wanafunzi wa Sekondari ya Myovizi waliohudhuria mafunzo hayo wamesema elimu hiyo iwafikie mara kwa mara kwani inawakumbusha namna ya kujilinda na kuendelea kufanikisha ndoto walizonazo.



Comments
Post a Comment