JINSI NA KAMATI YA USALAMA NA TRA ZILIVYOFANIKIWA KUKAMATA BIDHAA ZA MAGENDO ZIKIWEMO SILAHA NA PEMBE ZA NDOVU SONGWE.
MAKALA
-VIPENYO ZAIDI YA 300 VYA KUPITISHIA BIDHAA ZA MAGENDO KAA LA MOTO,SERIKALI YATOA MAGARI 6 KUONGEZA NGUVU BAADHI YA ASKARI WATIWA KOLOKOLONI WAKIHUSIKA.
RIPOTI MAALUM
Na Ibrahim Yassin,Songwe
IMEELEZWA kuwa vipenyo zaidi ya 300 vilivyopo wilaya ya Ileje kupitia mwambao wa mto Songwe na maeneo ya mapori katika mpaka wa Nakonde Zambia na Tunduma Tanzania imekuwa kaa la moto baada ya mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) na kamati ya usalama kuongeza udhibiti.
Mpaka wa Tunduma ni lango la nchi za kusini mwa afrika (SADC) ambapo asilimia 70 ya bidhaa zinazovuka kutoka bandari ya Dar es salaam zinapitishwa kwenye mpaka huu hali inayoongeza pato kubwa la Taifa la zaidi ya Bilioni 200.
Kutokana na mpaka huu kuchangamka imekuwa ni kimbilio la vijana kutoka mikoa mbalimbali nchini na hata nje ya nchi hukimbilia kuja kufanya shughuri mbalimbali za kujiingizia kipato huku wengine wakikosa uaminifu wakitumia njia za panya kupitisha mizigo.
Mkoa huu wa Songwe kupitia mpaka wa Tunduma umepakana nan chi za Malawi kwenye wilaya ya Ileje na nchi ya Zambia upande wa Tunduma wilayani Momba ambao umekuwa ukikua kila siku kutokana na uwingi wa watu wanaofika kufanya shughuri za usalishaji.
Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikiweka makadirio kadhaa ya ukusanyaji mapato lakini imekuwa ikivuka lengo la makusanyo kutokana na ushirikiano mzuri baina yao na wafanya biashara ambao wamekuwa wakikaa nao na kuelezea mambo mbalimbali.
Ushirikiano huo umefika hadi kwa wananchi hasa wanaoishi pembezoni mwa mipaka hiyo wakielezwa kuwa wazalendo kuwafichua wanaokwepa kodi wakitumia njia za panya kupitisha mizigo wengi wao wakificha kwenye nyumba zao.
Elimu hiyo imekuwa na mafanikio ya kuweza kukusanya mara dufu mapato kwani mwaka 2021-2022 walikadiria kukusanya Bilioni 66 lakini walivuka lengo kwa kukusanya Bilioni 84,lakini makusanyo hayo yalivuka zaidi baada ya elimu na kufikia Bilioni 186 mwaka 2024-2025 na kuvula lengo Bilioni 204.
Hata hivyo imeelezwa kuwa makusanyo hayo ni baada ya kuendesha operesheni mbalimbali kupitia njia hizo za mpenyo (Za Panya) zilizoleta matunda kwa kuwakamata watu kadhaa wakivusha bidhaa zikiwemo pembe za ndovu na silaha.
Pia matunda ya operesheni zilizofanyika zimeleta matunda baada ya kukamata fedha za kimarekani zenye thamani ya Tanzaniazenye thamani ya zaidi ya milioni 40 na kukamata pembe za ndovu zenye thamani ya Milioni 240, zikiwemo dawa za kulevya aina ya bangi na milungi,silaha aina ya bastola na magobole,zikiwa na risasi,Mbolea,dawa za magugu,sukari,uyo ga,mayai ya kisasa na bidhaa zinginezo.
Meneja wa Forodha mkoani Songwe Nsajigwa Mwambegele, anasema kulikuwa na changamoto mbalimbali za watumishi na vitendea kazi,ambapo Kamishiana wa TRA Yusuph Mwenda aliweza kuwapatia magari na watumishi.
Anasema magari hayo waliweza kuongeza doria wakishirikiana na kamati za usalama ya wilaya na mkoa na kufanikiwa kukamata shehena nyingi za mizigo ikiwemo mbolea za wizi zilizokuwa zikivushwa kwenda nchini Malawi maeneo ya Tazara.
Anasema vipenyo hivyo 300 vilidhibitiwa na kufanikiwa kukamata Mbolea,dawa za kuulia magugu,mafuta ya taa na kupikia,vipodozi,mayai ya kisasa na bidhaa zinginezo ambapo hali hiyo ya opelesheni baadhi ya wafanya biashara wameanza kupita njia za halali wakilipia bidhaa kuwepa kukamatwa.
Anasema bidha mfano mafuta yakikamatwa serikali inataifisha alafu maafisa wa chakula na dawa wanazitekeketa kwa kuzichoma moto,mbolea ikitaifishwa maafisa wa wakala wa chakula wanazigawa kwenye taasisi ikiwemo Jeshi la Magereza au watoto yatima.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake,kamanda wa polisi mkoani Songwe Augostino Senga,anasema kwa kushirikiana na maafisa wa mapato mkoa wameweza kufanikiwa kukamata bidhaa mbalimbali hali iliyopunguza uvushaji wa magendo.
Anasema kwa kipindi cha mwezi Januari 2024 hadi sasa Mwezi Septemba 2025 kea wilaya ya Momba kupitia mpaka wa Tunduma Tanzania na Nakonde Zambia,polisi wakiwa katika doria wamefanikiwa kukamata watuhumiwa kadhaa wakivusha bidhaa.
Anasema watuhumiwa hao ni Fredy Katete na wenzake wawili wakiwa na vitenge vya Zambia belo 26 wakiingiza nchini bila kulipia,wakitumia gari namba T.519 DAE/ T834 AGZ aina ya Fawn na T546,DSL Toyota Hice ambapo watuhumiwa walikabidhiwa kwa uongozi kwa hatua za kiforodha.
Anasema wakiwa katika msako pia walifanikiwa kumkamata Melkamu Getachew na wenzake 4 Raia wa Ethiopia walioingia nchini bila vibali,na pia katika eneo la Sikanyika Momba walifanikiwa kumkamata Huruma Kennedy Raia wa Burundi aliyeingia nchini bila kibali ambao walikabidhiwa idara ya uhamiaji.
Kamanda Senga anasema operesheni hiyo iliendelea na kuleta mafanikio baada ya kukamata betri za simu,noti bandia aina ya Kwacha za nchini Zambia,aina mbalimbali za vipodozi,nyavu za kuvulia samaki nchi mbili nan chi mbili na robo zilizoingizwa nchini kwa kutumia pikipiki isiyokuwa na namba za usajili,
Aidha anasema walifanikiwa pia kukamata boksi 194 za vipodozi mbalimbali vilivyoingizwa nchini kinyemela na pia walikamata pombe za vifungashio vya plastiki (Viroba) aina ya Ginja paketi 192 zilizopigwa marufuku kuingizwa nchini.
Anasema operesheni eneo la Tunduma kati na Black mpaka waTanzania na Zambia,hizo ziliendelea na kufanikiwa kukamata silaha aina ya bastola CZ92 Browning namba A 428007 Cariber 6,35MM ikiwa na Risasi 6 ndani ya Magazine iliyokuwa ikitafutwa baada ya kuibwa wilayani Momba April 13 2025.
Na pia mafanikiwa ya msako mungine ni kukamata Bastora Retay G19C yenye namba R1YGCMOY501-2400425 CAL 9MM Ikiwa na Risasi 150 ndani ya boksi ambayo ilitelekezwa baada ya mtuhumiwa kukimbilia upande wa Zambia,pia walikamata kobole likiwa na silaha 3 lilitengenezwa kienyeji.
Na pia Kamanda Senga anasema vijana wake wakishirikiana na maafisa wa TRA na TFS (Misitu) walifanikiwa kumkamata Husein Juma akiwa na fedha Dola 160 za marekani sawa na Milioni 400 za Tanzania zikiwa kwenye maungo yake bila kufuata utaratibu wa kisheria ambapo upelelezi unaendele.
Kamanda Senga anasema vijana wake wakishirikiana na mamlaka ya mapato (TRA) walifanikiwa kukamata pikipiki namba MC367 EAE ikiwa imebeba katoni za sukari,mayai ya kisasa ba Uyoga ukitokea nchini Malawi,na moja na pikipiki namba MC 981 DSV ikibeba bidhaa za magendo.
Na pia walikamata pikipiki namba MC 112 CHU ikiendeshwa na Kefas Mwashilindi ikiingiza bidhaa nchini zikitokea nchini Malawi bila kulipia na pia pikipiki zaidi ya 20 zilikamatwa zikivusha bidhaa za magendo kutoka nchini Malawi ambapo watuhumiwa wote walikabidhiwa TRA kwa taratibu zingine za kisheria.
‘’Ndugu mwandishi hivi juzi tu vijana wangu wakiwa katika doria wakishirikiana na maafisa wa TRA walifanikiwa kukamata Mbolea ya Urea mifuko 403 yenye zaidii ya Milioni 28,613,000 na Dap mifuko 130 yenye thamani ya zaidi ya Milioni 8,580,000 zilizokuwa katika harakati za kuvushwa kwenda nchini Zambia.
Hata hivyo Kamanda Senga anasema pia vijana wake walifanikiwa kukamata vipande 18 vya pembe za ndovu ambavyo thamani yake bado haijapatikana …….
Anasema hayo ni mafanikio makubwa yaliyofanywa na jeshi la polisi wakishirikiana na maafisa wa mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) na kuwa serikali imewaongezea nguvu kwa kuwapatia magari 6 ya kisasa yatakayotumika kwa kazi hiyo.
Anasema lengo kuu la serikali ni kuongeza mapato na kuondoa uharifu, na wao kama jeshi la polisi watahakikisha wanaendesha operesheni kila siku na kuwatia hatiani wanaobainika kuvunja sharia zilizopo.
WASEMAVYO WAFANYABIASHARA.
Samwel Mtafya mkazi wa Ileje anasema jeshi la polisi linafanya kazi kubwa usiku na mchana kudhibiti uharifu na uingizaji au uvushaji bidhaa kwa njia za magendo na kuwa Ileje kupitia mto Songwe umekuwa ukitumika kuvushia bidhaa hivyo jitihada zaidi ziongezwe.
Anasema wafanyabiashara wengi wanaopita njia za panya kuvusha bidhaa wanapata faida mara dufu,kwenye chenji na kwenye mizigo,mfano elfu 10 yaTanzania ikibadirishwa inakuwa na thamani kubwa nchini Malawi, ikibadirishwa kuwa kwacha ikinunuliwa mzigo na kuvushwa Tanzania.
Nae Jumanne Sichizya mkazi wa Momba anasema amekuwa akishuhudia jeshi la polisi wakiwa na maafisa wa TRA wakiendesha diria na kufanikiwa kuwakamata watu wanaovusha bidhaa kwa njia za magendo jitihada zaidi zinahitajika kuhakikisha kila mfanyabiashara analipia mizigo na kupita njia kuu.
Mpaka huo wa Tanzania na Zambia unatumiwa na Nchi zote za kusini mwa Afrika (SADC) ambao ni jicho la serikali kutokana na mapato makubwa yanayopatikana,mbali na kazi kubwa iliyofanywa na serikali kupitia mamlaka hizo,jitihada zaidi zinahitajika kuongeza udhibiti ili mapato yaongezeke zaidi.
Mwisho..mwandishi wa Ripoti hii anapatikana kwa simu namba 0715869996/0758269996 barua pepe yassin.ibrahimu@yahoo.com




Comments
Post a Comment