Wananchi wahamasishwa matumizi ya lishe bora kulinda afya
Na Israel Mwaisaka,Nkasi
Katika kukabiliana na changamoto za kiafya zinazotokana na lishe duni Wataalamu wa afya wameyatumia maadhimisho ya siku ya afya na lishe ya kijiji katika kutoa elimu ya lishe ikiwa ni pamoja na kuwapatia vipimo mbalimbali vya kiafya Ili kufahamu hari za afya zao.
Akizungumza na Wananchi wa kijiji cha Majengo afisa lishe wa wilaya Nkasi Theresia Matoke amesema kuwa bado Kuna changamoto kubwa ya lishe katika jamii na kuwa kutokana na Hilo ndiyo maana wao wameamua kuitumia siku hiyo ya afya na lishe ya kijiji katika kutoa elimu mahususi kwa nadharia na vitendo.
Amezitaja changamoto za kilishe kuwa ni utapiamlo,upungufu wa virutubisho, vitamin na madini na kupeleka kukosekana kwa damu na Wanawake kupata shida wakati wa kujifungua ikiwa ni pamoja na uzito uliopitiliza unaosababisha magonjwa ya yasiyo ya kuambukiza.
Matoke ameitumia siku hiyo kuitaka jamii kuhakikisha kuwa inajenga utamaduni wa kupima afya zao Kila wakati ikiwa ni pamoja na kuthibitisha kwamba chakula wanachokula kina viini lishe muhimu Ili kuweza kulinda afya zao.
Richard Kauzeni mratibu wa magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza ameitaka jamii kuwa na ratiba sahihi ya kupata chakula sahihi ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi ya kutosha Ili kuweza kukabiliana vilivyo na changamoto hiyo ya magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza.
Amesema kwa sasa magonjwa yasiyo kuwa ya kuambukiza yamekua ni sehemu ya janga kubwa Katika jamii hivyo ni muhimu kwa sasa kufuatilia kanuni za lishe bora katika kukabiliana na changamoto za namna hiyo
Mratibu wa bima ya afya Stanley Joseph kwa upande wake ameitaka jamii kujiunga na mfuko wa bima ya afya ya jamii CHIF na kuwa bima ya afya ni Moja ya vitu muhimu katika kukabiliana na maradhi pindi yatokeapo kwa maana bima inakupa uhakika wa matibabu wakati wote
Mkuu wa wilaya Nkasi Peter Lijualikali kwa upande wake aliwataka Wananchi kutumia vyema vyakula wanavyozalisha kwa kuhakikisha wanakula vyakula kama ilivyo maelekezo ya wataalamu wa afya




Comments
Post a Comment