NKASI YAPATA HATI SAFI RC MAKONGORO APONGEZA
Na Israel Mwaisaka,Rukwa
MKUU wa Mkoa Rukwa Charles Makongoro Nyerere ameipongeza halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kwa kupata hati safi na kuwa hicho ni kielelezo cha ushirikiano mzuri kati ya watendaji wa halmashauri ,madiwani na wadau wengine katika kuona halmashauri inasonga mbele.
Pongezi hizo amezitoa leo Juni 11,2025 kwenye kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kuhusu utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kwa mwaka 2023-24 ambapo amesema kuwa katika msimu uliopita kulikua na hoja nyingi za ukaguzi lakini kwa sasa zimepungua mno na kuona kwamba kuna kitu kinafanyika ndani ya halmashauri.
Amesema kuwa amefurahishwa na namna ambavyo imekuwa ikijishughulisha na ufutaji wa hoja mbalimbali zilizojitokeza kwa kutolea mfano kuwa kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Aprili 2025 halmashauri ya wilaya Nkasi ilionyesha kuwa na hoja za miaka ya nyuma 21 na hivyo kufanya kuwa na hoja 38 na maagizo 4 yenye vipengele 10 ya kamati ya kudumu ya bunge ya hesabu za serikali (LAAC) ambapo maagizo hayo mengi yapo katika ya utekelezaji na hoja nyingi kufutwa.
Kufuatia hali hiyo Mkuu huyo wa Mkoa amependa kusisitiza baadhi ya hoja ambazo inatakiwa kufanyika kwa haraka kuwa ni mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mwaka 2023/24,usimamizi wa manunuzi na miradi ya maendeleo,usimamizi wa Rasilimali watu na mali za halmashauri,usimamizi wa matumizi ,upimaji wa ufanisi na utekelezaji wa mpango na bajeti
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa Msalika Makungu amekiri kuwepo kwa mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika halmashauri ya wilaya Nkasi na kuwa kitendo cha kupata hati safi ni kitu ambacho kilistahili kwa namna walivyoamua kushirikiana kwa pamoja katika kuona halmashauri yao inasonga mbele.
Alidai kuwa siri ya mafanikio mahala popote pa kazi ni ushirikiano na kufuata kanuni za kiutendaji na kuwa na malengo ya pamoja katika kuyafikia mafanikio waliyoyalenga
Mkuu wa wilaya Nkasi Peter Lijualikali amesifu ushirikiano mkubwa uliofanywa na Madiwani katika kuwa pamoja na watendaji wa halmashauri na kuwa hicho ndiyo siri kubwa ya mafanikio miongoni mwao.
Akihitimisha Baraza hilo mwenyekiti wa Halmashauri Pankrasi Maliyatabu amemweleza mkuu huyo wa mkoa kuwa Madiwani wanamaliza msimu wao wa kiuongozi mwaka huu na kuwa wanaiacha halmashauri ikiwa katika mazingira mazuri na salama katika kutoa huduma huduma kwa wananchi.





Comments
Post a Comment