Na Israel Mwaisaka,Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere amewaongoza mamia ya wafanyakazi Mkoani Rukwa katika sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) zilizofanyika jana Mei 1, 2025 kimkoa katika mji wa Matai Wilayani Kalambo huku akiwakumbusha wajibu wao wa msingi.
Akiwahutubia wafanyakazi na wananchi waliohudhuria, Makongoro amewataka waajiri kuheshimu haki za wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara kwa wakati, kutoa mikataba ya aWAjira, na kuwarejesha wastaafu makwao kwa wakati.
Makongoro amewataka waajiri kufanya vikao vya mabaraza ya wafanyakazi kwa wakati na kuagiza Sekretarieti ya Mkoa kusimamia utekelezaji wa agizo hilo kwa mujibu wa Sheria.
Aidha, ameielekeza Idara ya Kazi kuwafuatilia waajiri wa sekta binafsi wanaokiuka masharti ya ajira na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo kwa Katibu Tawala wa Mkoa mapema iwezekanavyo.
Mkuu huyo wa Mkoa pia ametumia fursa ya maadhimisho hayo kuhamasisha wananchi kushiriki zoezi linaloendelea la uboreshaji wa daftari la kudumu la
wapiga kura. Zoezi hilo linatarajia kukamilika Mei 7, 2025.
Kauli mbiu iliyobeba maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Mwaka 2025 ni; “Uchaguzi Mkuu 2025 Utuletee Viongozi wanaojali na kuthamini haki na maslahi ya wafanyakazi – sote tushiriki.”
Comments
Post a Comment