WAANDIKISHAJI WAPIGA KURA WATAKIWA KUFANYA KAZI YAO KWA UWELEDI ILI KUFANIKISHA JUKUMU HILO LA KITAIFA
Na Israel Mwaisaka,Nkasi
WASHIRIKI wa mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili wametakiwa kufanya kazi yao kwa ueledi mkubwa ili kuweza kufanikisha jukumu hilo la msingi la kitaifa na kuhakikisha wale wote wenye sifa wanajiandikisha katika daftari hilo.
Wito huo umetolewa jana na afisa mwandikishaji wa wilaya Nkasi Ladislaus Mzelela alipokuwa akifunga mafunzo ya siku moja kwa maafisa Waandikishaji wasaidizi na waendesha vifaa ambapo amedai kuwa jukumu lao ni kubwa hivyo uweledi pekee utapelekea kufanikisha kazi hiyo kwa ufanisi.
Alisema kuwa mafunzo hayo waliyoyapata kwa njia ya nadharia na vitendo yalijikita katika ujazaji fomu mbalimbali zitakazotumika vituoni fomu za kiapo cha kutunza siri na kujitoa uanachama katika chama cha siasa ikiwa ni pamoja na namna ya kuandikisha wapiga kura wapya,wanaorekebisha au kuboresha taarifa zao ikiwa ni pamoja na wale wanaoondolewa au kufutwa kwenye daftari la kudumu la mpiga kura.
Hivyo amewataka kutambua uzito na umuhimu wa zoezi hilo la kitaifa na kwa kuwa wameelewa mafunzo hayo kwa kina hivyo elimu na ujuzi walioupata ikawasaidie kutekeleza jukumu hilo la msingi katika kuhakikisha wale wote wenye sifa stahiki wanapata nafasi ya kuandikishwa katika daftari la kudumu la mpiga kura.
Mzelela amewataka waandikishaji hao kutambua kuwa wanalo jukumu na madaraka makubwa katika vituo vyao vya kuandikisha na kuwa kazi ikienda mrama uadilifu wao utatiliwa mashaka na athari zake zitatikisa taifa.
Pia amewataka Wananchi kujitokeza kwenda kujiandikisha kwenye daftari hilo kuanzia Mei 1,2025 zoezi ambalo litadumu kwa muda wa siku saba.
afisa uchaguzi wilaya Nkasi Atufigwege Mwakitega kwa upande wake aliwataka maofisa hao waandikishaji kuhakikisha wanavitunza vyema vifaa watakavyokabidhiwa kwa ajiri ya kazi hiyo na kuwa kazi hiyo ili iweze kuleta tija inategemea vifaa hivyo kwa maana hiyo kuna sababu za kuvitunza vifaa hivyop kwa umakini mkubwa.
Na aliwataka waandikishaji katika vituo watakavyopelekwa kuhakikisha kwamba wanakua na tabia njema na busara kitu ambacho kitahakisi kazi njema waliyotumwa na tume huru ya taifa ya uchaguzi na kuwaomba kutojihusisha na vitendo vya ulevi katika kipindi chote cha siku 7 watakapokuwa wakitekeleza jukumu hilo kubwa na la msingi.
Washiriki wa mafunzo hayo waliahidi kwenda kuifanya kazi hiyo kwa weredi mkubwa na kuwa kila walichojifunza watakifanya kwa vitendo ili kila mmoja mwenye haki ya kuandikishwa anaandikishwa kwa mujibu wa sheria
Mwisho




Comments
Post a Comment