VIONGOZI WA DINI WAKERWA NA MANENO YA KUSUSIA UCHAGUZI
Na Israel Mwaisaka,Nkasi
JUMUIA ya Maridhiano na amani (JMAT) wilayani Nkasi mkoani Rukwa inayoundwa na viongozi wa dini mbalimbali wameitaka jamii kutosikiliza maneno mbalimbali yanayotolewa na baadhi ya watu juu ya kuzuia uchaguzi na kuwa maneno hayo yana madhara makubwa na badala yake watafute namna nzuri na sahihi ya kusuruhisha jambo hilo badala ya kuzuia uchaguzi usiwepo.
Akizungumza kwenye kikao chao cha kawaida Mwenyekiti wa jumuia hiyo Sheikh wa wilaya Nkasi Hadhiri Daruweshi amedai kuwa neno la “No reform no election) linaweza kuonekana ni neno dogo na kuwasihi viongozi wa dini katika maeneo yao kuhakikisha wanaijenga jamii wanayoizunguka na kuyakataa maneno hayo ambayo yanaweza kuleta mpasuko mkubwa katika taifa utakapofika wakati wakati wa uchaguzi.
Aliwataka wanaoeneza sumu ya kutofanyika kwa uchaguzi kutafuta namna iliyo njema kwa kukaa na serikali kuona namna ya kurekebisha yanayodaiwa ili ifikapo oktoba ya mwaka huu wa 2025,wananchi washirriki uchaguzi mkuu na kuweza kuwapata viongozi watakaowatumikia Wananchi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
“nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa sheria na kanuni hivyo ni vizuri changamoto zikazungumzwa kisheria na namna ya kuzitatua lajkini kuibuka na kusema tutazuia uchaguzi siyo sawa na kuweza kuleta hatari ya machafuko kitu ambacho hatukitaki kitokee” alisema
Hivyo aliwaomba viongozi hao wa dini katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba ya mwaka huu kuhakikisha kwamba wanafanya maombi ya kuliombea taifa na viongozi wake kila wakati ili taifa liendelee na utengamano uliopo.
Katibu wa jumuia hiyo Mch,Fidelis Maheke kwa upande wake amesisitiza kuwa suluhisho la amani iliyopo sasa Nchini ni kuendelea kuliombea taifa kwa nguvu na kuwa uwezo huo kama viongozi wa dini wanao.
Pia amedai kuwa uwezo wa kuzuia mihemko ya vijana juu ya kufanya mambo yanayoweza kwenda kinyume na sheria kama vurugu na mengineyo ni rahisi kwao kuweza kuvizuia na kuwa wasipuuze kila jambo linaloonekana kwenda kinyume na maadili na wawe tayari kukemea mabaya kila yanapojitokeza.
Mdau wa maendeleo wilayani Nkasi Salum Kazukamwe aliitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa dini kuhakikisha suala la elimu linapewa kipaumbele katika jamii kwani silaha ya maendeleo katika jamii yopyote ni elimu.
Alidai wao kama viongozi wa dini jukumu hilo wanaliweza na kuwa hata katika nyumba za ibada kunapokuwa na wasomi wengi ni rahisi sana kwa makanisa na misikiti wanayoiongoza kupiga hatua kubwa za maendeleo.
“Elimu ndiyo silaha kubwa kwa kila mmjo hivyo ninyi kama viongozi wa dini mnaweza mkalisimamia hilo na kuweza kuleta matokeo chanya’’
Awali wakati akifungua kikao hicho mwakilishi wa mkuu wa wilaya Nkasi Kassim Mfangavo aliwataka viongozi hao kusimamia maadili kwa watu wanaowaongoza na kuitangaza amani tuliyonayo kwa nguvu huku wakieleza madhara yanayoweza kujitokeza pale amani inapoyumba.


Comments
Post a Comment