Mvua yenye upepo mkali yasababisha maafa nyumba zabomoka, familia zakosa makazi
Na Israel Mwaisaka, Nkasi
Nyumba 29 zimebomoka na nyingine kuezuliwa para kufuatia mvua yenye upepo mkali katika vijiji vya Mabatini na Mkangale kata ya Namanyere huku familia kadhaa zikiachwa bila ya makazi.
Diwani wa kata ya Namanyere Nestory Kaloto akitoa taarifa mbele ya kamati ya maafa ya wilaya ikiongozwa na mkuu wa wilaya Nkasi Peter Lijualikali amesema kuwa tukio Hilo limetokea juzi jioni baada ya mvua iliyokuwa imeambatana na upepo mkali kunyesha na kusababisha maafa hayo.
Amesema kuwa wengi wao wanahifadhiwa na majirani zao na kuwa wengi wanahitaji msaada mkubwa na wa haraka Ili kuweza kurudia katika hari Yao ya kawaida.
Mkuu wa wilaya ambaye pia ndiye mwenyekiti wa kamati ya maafa ya wilaya Peter Lijualikali kwa upande wake amewataka wakazi wa eneo Hilo kupanda miti ya kutosha Ili kukabiliana na changamoto hiyo Na kuwa ameagiza halmashauri kupeleka mara Moja Miche ya miti mbalimbali Ili waanze kuipanda miti hiyo.
Pia amewataka kufuata kanuni za ujenzi pale wanapoanza kujenga nyumba Ili kuweza kujenga nyumba zenye ubora zinazoweza kukabiliana na changamoto kama hizo ili ziweze kukabiliana na dhoruba kama hizo.
Kaimu mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya Nkasi Mayuma Zilantuzu kwa upande wake amesema kuwa kuanzia kesho Miche ya miti itafika huko Ili Watu waendelee kuipanda miti hiyo hasa katika kipindi hiki chenye mvua za Masika.
Awali baadhi ya Waathirika wa mvua hiyo wameiomba serikali Ione namna ya kuwasaidia kwa haraka kwani hari zao siyo nzuri kutokana na vitu vyao vingi kuharibiwa na mvua Baada ya nyumba zao kubomolewa.
Pia kamati hiyo ya maafa ilikabidhi msaada wa vifaa vya ujenzi kwa mhanga wa moto Beatrice Makoloka mkazi wa Mabatini ambaye nyumba yake iliungua kutokana na hitilafu ya umeme ambavyo ni Mbao PC 15 zenye thamani ya shilingi 10,500,misumari Kg 5,Saruji mifumo 4 pamoja na bati 8 ambapo vyote vina thamani ya Tshs,370,000



Comments
Post a Comment