Mtandao wa Polisi Wanawake TPF-Net Nkasi wafanya matendo ya huruma kuelekea siku ya Wanawake duniani



Na Israel Mwaisaka,Nkasi

MTANDAO wa Polisi Wanawake wilayani Nkasi mkoani Rukwa TPF-NET limeafanya matendo ya huruma kwa kuwatembelea wagonjwa katika hospitali ya wilaya Nkasi na kuwapatia zawadi mbalimbali kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani.

Akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo kwa wagonjwa mwenyekiti wa mtandao wa Polisi wilayani Nkasi Ivona Mwanga amesema kuwa katika kuelekea kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani March 8 wao wameonelea kufanya matendo hayo ya huruma kwa kuwapatia zawadi mbalimbali huku wakitoa ujumbe mahususi juu ya siku ya Wanawake duniani.



Amesema kuwa TPF-Net kama mtandao wa Polisi Wanawake umeundwa kwa ajili ya kuisaidia jamii katika kukabiliana na vitendo mbalimbali vya ukatili katika jamii na kuwataka Wananchi kutokaa kimya pale wanapoona wanaonewa bali wakimbilie Polisi ambako lipo dawati la jinsia na Watoto ambako wanaweza kupata haki zao za kimsingi

Katibu wa mtandao huo Anna kisimba kwa upande wake ameitumia siku hiyo kutoa elimu kwa jamii na kutaka kulitumia dawati la jinsia la jeshi la Polisi katika kudai haki zao za msingi.

Amedai kuwa wao kama Polisi Wanawake wamejikita zaidi katika kuhakikisha makundi mbalimbali katika jamii yanapata haki sawa bila ya kujali jinsia na kubwa ni la kuhakikisha jamii inaishi kwa amani na utulivu.



Mkuu wa kituo cha Polisi Namanyere ambaye pia alimuwakilisha mkuu wa Polisi wa wilaya Francis Mabisi amesema kuwa wao walionelea katika maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani mwaka huu kuiadhimisha kwa kushirikiana na jamii yenye uhitaji hasa wagonjwa kwa kuwapatia misaada midogo ya kijamii kama sehemu ya kusogeza huduma za Kipolisi kwa jamii na kujenga mahusiano katika kukabiliana na vitendo mbalimbali vya uhalifu na kubwa kukabiliana na vitendo vya ukatili.



Afisa ustawi wa jamii katika hospitali ya wilaya Nkasi Jackson Bolingo amewashukuru Polisi Wanawake wa wilaya Nkasi kwa kuwa na maono ya kuwatembelea wagonjwa katika hospitali hiyo na kuwa kwa kitendo hicho wanaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa jeshi la polisi katika kukabiliana na vitendo mbalimbali vya uhalifu

Maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani mwaka huu yamebeba ujumbe mahususi usemao : Wanawake na Wasichana 2025 Tuimarishe haki,Usawa na Uwezeshaji.

Comments

Popular posts from this blog

KAEGELE NA KAZUKAMWE WAIBUKA KIDEDEA KURA ZA MAONI CCM WILAYANI NKASI

DIWANI KATA YA KALA AFARIKI DUNIA KWA UGONJWA WA KIHARUSI

Mke wa Mchungaji wa kanisa la EAGT ajinyonga akihofia deni lake la fedha za kanisa