RC RUKWA-MIRADI YA MAENDELEO ITEKELEZWE KWA KASI KUBWA NA VIWANGO VINAVYOKUBALIKA
Na Israel Mwaisaka,Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa,Charles Makongoro Nyerere, amezitaka Halmashauri zote Mkoani hapa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Makongoro ametoa maelekezo hayo jana, Januari 07, 2025, wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya ujenzi wilayani Nkasi.
Miradi iliyokaguliwa Wilayani Nkasi katika ziara hiyo ni ujenzi wa Shule ya Amali ya Mkoa, Shule mpya ya Msingi Chala Kima pamoja na ujenzi wa mabweni na madarasa katika Shule ya Sekondari Chala.
Mkuu wa Mkoa amesema kuwa ni jukumu la kila Halmashauri kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati na kwa viwango huku akiwataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuongeza jitihada katika usimamizi wa miradi kwa kuhakikisha kazi zinaendelea usiku na mchana ili kufanikisha malengo yaliyowekwa.
Ziara ya Mkuu wa Mkoa inalenga kuhakikisha kuwa fedha za miradi ya maendeleo zinatumika ipasavyo na miradi yote inatekelezwa kwa kuzingatia muda na viwango vya ubora vilivyowekwa.



Comments
Post a Comment