Waandishi wa habari wapewa mbinu ya kuutangaza urithi wa kiutamaduni ili ulete manufa kwa jamii
Na Israel Mwaisaka,Rukwa
WAANDISHI habari na wadau mkoani Rukwa wametakiwa kutumia kalamu zao katika kuuhamasisha urithi wa Utamaduni usioshikika Ili kuweza kutoa mchango Kwa taifa kulingana na tamaduni hizo.
Akitoa taarifa Kwa mkuu wa wilaya Sumbawanga Nyakie Chirukie kwenye ufunguzi wa Warsha ya siku mbili Kwa Waandishi wa habari mkurugenzi wa Taasisi ya TAMCODE Rose Ngunangwa amesema kuwa hivi Sasa Kuna tamaduni nyingi zenye manufaa Kwa jamii zimeachwa lakini kama zikiendelezwa na kurithishwa zinaweza kuleta Tija.
Alisema kuwa katika maeneo mbalimbali hasa katika mikoa ya Rukwa na Katavi yapo maeneo muhimu ambayo ni urithi wa kitamaduni usioshikika na kuwa maeneo hayo yakitambuliwa na kurithishwa tamaduni hizo zinaweza kuwa na mchango hata katika eneo la kiuchumi.
Ngunangwa alidai kuwa Bado Kuna fursa kubwa ya kiuchumi kwenye tamaduni zetu na ndiyo maana wao TAMCODE Kwa kushirikiana na Mradi wa UNESCO-Alwaleed Philanthropies wameamua kufanya uchechemuzi Kwa Waandishi wa habari Ili waweze kuwa msaada Kwa jamii katika kuzitangaza tamaduni zetu zenye urithi mkubwa.
Alifafanua kuwa Kuna shughuli nyingi za kitamamaduni ambazo jamii wanaweza kuzifanya na kuweza kujipatia kipato,hivyo ni muhimu sana Kwa tamaduni zenye manufaa kuendelezwa Ili jamii iendelee kupata manufaa ya Mila na tamaduni zetu ambazo Kwa Sasa zimepuuzwa.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Nyakie Chirukie amewapongeza TAMCODE Kwa kushirikiana na UNESCO Kwa kuanzisha mchakato huo kwani ni kweli Kwa Sasa jamii yetu imejisahau kabisa katika kuzitumia tamaduni zetu ambazo Bado Zina manufaa makubwa.
Alisema kuwa Kuna vitu vingi vya kitamaduni ambavyo vimesahaulika kabisa na hata kufikia wakati jamii imesahau hata vyakula vya asili kitu ambacho ni hatari Kwa vizazi vijavyo.
Alisema mkoa wa Rukwa una vitu vingi ambavyo ni urithi wa kitamaduni tumeachiwa ikiwemo ugunduzi wa Herrium ambayo ni nyingi,ulinzi wa misitu yetu ambayo tunaweza kunufaika na biashara ya hewa ukaa na kuwataka Waandishi wa habari kuibeba ajenda hiyo Kwa uzito mkubwa Ili urithi wetu wa kitamaduni uweze kuendelea kutunufaisha.
Amedai kuwa mkoa wa Rukwa una Raslimali nyingi za kitamaduni ambazo ni urithi wetu ambazo hazijatangazwa vya kutosha na kuomba mafunzo haya yawe Chachu Kwa Wanahabari kuhakikisha wanatangaza vitu vyote ambavyo ni Raslimali yetu ya kitamaduni zijulikane kote Duniani na kuwa hiyo ndiyo njia pekee tunayoweza kunufaika na Raslimali hizo za kitamaduni.
Wanahabari Kwa upande wao wamesema kwamba wameibeba hiyo kama ajenda na kuomba Serikali kutoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa jukumu Hilo muhimu na kuwa Wana Imani kuwa jambo Hilo litatekelezeka vizuri.
Nyagazi George na Baraka Lusajo wameishukuru TAMCODE Kwa kushirikiana na UNESCO Kwa mafunzo hayo na kuwa watakwenda kuwa Waalimu Kwa Waandishi wengine ambao hawajahapata mafunzo hayo na kuwa na ajenda Moja ya kuuhamasisha urithi wa Utamaduni usioshikika.
Mafunzo hayo yamewashirikisha Waandishi wa habari wa radio jamii zote za mkoa Rukwa,Magazeti,TV,Bloggers,Online Media na mitandao mbalimbali ya kijamii.





Comments
Post a Comment