Serikali wilayani Songwe yaweka mkakati kuboresha uzalisha wa zao la tumbaku



Na Ibrahim Yassin,Songwe.

Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Mhe. Solomon Itunda amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa kilimo cha Tumbaku kujadili mikakati ya kuboresha uzalishaji wa zao hilo kwa msimu wa 2024/2025.

Mazungumzo hayo yalifanyika jana kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya iliyopo Mkwajuni ambapo walikubaliana kufanya utafiti kubaini mbolea inayoendana na udongo kwenye eneo hilo.


Mbali na hilo pia walijadili mambo mengi ikiwemo kupeana elimu ya kilimo na matumizi ya pembejeo za kilimo kwa wakulima.

Akizungumza mara baada ya kikao hicho, Mhe. Itunda amesema kuwa Wilaya hiyo inatarajia kupata zaidi ya kilo 3.6 milioni kwa msimu wa kilimo wa 2024/2025.



Amewataka maafisa ugani kuhakikisha wanawafikia wakulima ili wawape elimu na ushauri wa kitaalamu utakaoleta matokeo yenye tija kwa wakulima wa zao hilo.

Hata hivyo, Mhe. Itunda amemshukuru Rais wa JMT, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuingiza zao la tumbaku kwenye pambejeo za mbolea za ruzuku na kutoa vitendea kazi kwa maafisa ugani zikiwemo pikipiki pamoja na vishkwambi kwaajili ya kukusanyia takwimu za wakulima.


Katika kikao hicho, Mhe. Itunda amekutana na wawakilishi kutoka TFC, Afisa Kilimo Mkoa wa Mbeya na Wilaya ya Chunya, wawakilishi wa CHUTCU, TFRA pamoja na Afisa Kilimo wa Wilaya ya Songwe.

Ifahamike kuwa wilaya ya Songwe katika Kata ya Gua ni maarufu kwa kilimo cha Tumbaku hivyo mkuu wa wilaya amefanya jambo zuri kujadili mikakati kuelekea msimu wa kilimo ili wakulima waongeze tija na kupata mazao mengi.




Comments

Popular posts from this blog

KAEGELE NA KAZUKAMWE WAIBUKA KIDEDEA KURA ZA MAONI CCM WILAYANI NKASI

DIWANI KATA YA KALA AFARIKI DUNIA KWA UGONJWA WA KIHARUSI

Mke wa Mchungaji wa kanisa la EAGT ajinyonga akihofia deni lake la fedha za kanisa