Afisa Mtendaji Ahukumiwa Kifungo cha Miaka 60 kwa Ubadhirifu wa Fedha

Na,Israel Mwaisaka,Nkasi

Mahakama ya Wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa, imemhukumu kifungo cha miaka 60 jela afisa mtendaji wa kijiji cha Paramawe, Richard Kiwela (45), kwa makosa matatu, ikiwemo kuibia Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kiasi cha shilingi 2,881,000 (Mil.2.8) alizokusanya kupitia mashine ya POS.

Mtuhumiwa alikabiliwa na mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu na kuisababishia hasara mamlaka, kinyume na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007 pamoja na sheria ya uhujumu uchumi. Mashitaka yalitolewa na mwendesha mashitaka wa TAKUKURU, Mzalendo Widege.

Mahakama ilipokea vielelezo 12 vilivyowasilishwa na upande wa mashitaka, ambavyo mtuhumiwa alikubali, hivyo kuimarisha kesi dhidi yake. Mwendesha mashitaka alieleza kuwa Kiwela alikabidhiwa mashine hiyo mnamo Novemba 11, 2018, na alikusanya jumla ya shilingi 55,825,600,  (Mil.55.8) lakini alishindwa kuwasilisha kiasi cha shilingi 2,881,000(Mil.2.8)

Hakimu mkazi mfawidhi, Denis Luwungo, alikubaliana na mashitaka hayo, akisema kuwa mtuhumiwa amekiri makosa yake. Kila kosa lilipewa adhabu ya miaka 20, ambapo mtuhumiwa ataitumikia kifungo hicho kwa pamoja. Ingawa ni kosa lake la kwanza, hakimu alisisitiza kuwa adhabu hiyo ni muhimu ili kuwa fundisho kwa watumishi wengine wa umma.

Kiwela aliiomba mahakama isimpatie adhabu kali, akidai kuwa yuko tayari kurejesha fedha hizo endapo mwajiri wake atamlipa. Upande wa mashitaka ulisisitiza umuhimu wa adhabu kubwa ili kuzuia uhalifu wa aina hiyo katika serikali.

Rufaa ipo wazi kwa siku 30 kwa mtuhumiwa endapo hataridhika na hukumu hiyo.

Comments

Popular posts from this blog

KAEGELE NA KAZUKAMWE WAIBUKA KIDEDEA KURA ZA MAONI CCM WILAYANI NKASI

DIWANI KATA YA KALA AFARIKI DUNIA KWA UGONJWA WA KIHARUSI

Mke wa Mchungaji wa kanisa la EAGT ajinyonga akihofia deni lake la fedha za kanisa