WAZAZI WANAOWATUMIA WATOTO KWENYE BIASHARA MUDA WA SHULE WAONYWA
Na Israel Mwaisaka,Nkasi
Afisa Ustawi wa jamii wilayani Nkasi mkoani Rukwa Oscar Mdenye amewaonya Wazazi wanaowatumia Watoto wao kufanya biashara za kuuza miwa katika stand kuu ya Namanyere muda ambao walitakiwa wawepo shule.
Onyo Hilo limekuja baada ya kubainika kuwepo Kwa Watoto ambao ni Wanafunzi muda wa kuwepo shule wakiwa wameambatana na Wazazi wao kwenye biashara mbalimbali mjini Namanyere ikiwemo biashara ya miwa na Watoto hao kukosa haki Yao ya kupata elimu.
Sambamba na Hilo afisa Ustawi huyo amewaonya wamiliki wa vibanda vya kuchezesha Magame kwenye Computer kutoruhusu Watoto kucheza michezo hiyo muda wa shule na kuwa atakayebainika atachukuliwa hatua Kali za kisheria.
Amefafanua kuwa hivi Sasa imebainika Watoto wengi majira ya asubuhi ukimbilia kujificha kwenye michezo hiyo ya Game na kutokwenda shule na wakati mwingine ulazimika kuiba fedha za Wazazi wao na kwenda kucheza michezo hiyo.
Amedai kuwa kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka Kwa Wazazi juu ya Watoto wao ambao wengi wao hawaonekani nyumbani na muda mwingi wanakuwepo kwenye vibanda vya Computer ambavyo wanacheza Magame hadi majira ya usiku kiasi Cha Watoto wengi wanaoshinda kwenye michezo hiyo wameshuka sana kitaaluma.
Mdenye amesema Kwa mujibu wa sheria ya mtoto ya mwaka 2019 inafafanua kuwa jukumu lote la malezi ya Mtoto ni la Wazazi ama Walezi na kukidhi mahitaji Yao yote na siyo kumtumia Mtoto kibiashara Kwa lengo la kutafuta kipato ni kwenda kinyume na sheria za Nchi.
Baadhi ya Wananchi waliozungumza na chombo hiki Cha habari walipongeza hatua hiyo iliyochukuliwa na serikali juu ya hilo na wao watakua mstari wa mbele katika kutoa taarifa pale wanapoona sheria inakiukwa Kwa kuwatumikisha Watoto kwenye shughuli za kiuchumi muda wa shule na kuwa Hilo halikubaliki.
Maria Mbalazi mkazi wa Kijiji Cha Mkole alidai kuwa wao kama Wazazi Moja ya jukumu lao ni kuhakikisha Watoto wao wanapata huduma zote za msingi na jukumu la kutafuta kipato Cha familia ni Cha mzazi na kuwa kuwapa majukumu ya utafutaji Watoto tena muda wa kuwa shule ni kuwanyima haki zao muhimu Watoto wanazotakiwa kuzipata.


Comments
Post a Comment