WANANCHI MPAPA WAHAMASISHWA KUUNDA SUNGUSUNGU KUNUSULU MAZAO NA MIFUGO KUIBIWA.



Na Ibrahim Yassin.Songwe 

IMEELEZWA kuwa ili kunusuru mazao yao hasa Ufuta kuibiwa shambani pamoja na mifugo ipo haja wananchi kuunda ulinzi shirikishi (Sungusungu) ili kulinda mali zao na kuwanasa wezi na kuwafikisha kwenye vyombo vya kisheria.

Kauli hiyo imetolewa leo August 6/2024 na mkulima bora wa Bonde la Kamsamba Abdul Ntila wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya kata ya Mpapa kupitia mikutano ya hadhara. 

Ntila amesema asilimia 80 ya wananchi wilayani Momba hasa wa bonde la Kamsamba wanategemea kilimo na ufugaji kuendesha maisha yao ya kila siku hivyo mkulima hapaswi kuchezewa.



Amesema masuala ya kilimo yanahitaji fedha na wengi wao huwa wanakopa kwenye taasisi za kifedha ama vikundi, hivyo mkulima anapovuna anahitaji auze bei nzuri na kulipa madeni kitendo cha kuiba mazao shambani kinaumiza wakulima.

"Kutokana na kukithiri kwa wizi wa mifugo na mazao nimezungumza na mkuu wa polisi kuhusu uundwaji wa Sungusungu, hivyo wananchi fanyeni kila muwezalo shirikisheni viongozi wenu ngazi za vijiji ulinzi uanze"amesema.

Ameongeza kuwa ni lazima mkulima ajiwekee mipango yenye tija ili kilimo kimtoe kwenye lindi la umasikini kuliko kuwategemea viongozi hasa wa kisiasa ambao hawana msaada na mkulima zaidi ya kumfanyia udalali.



Sambamba na hilo Ntila pia alishangaa kuona Meli kubwa zikibeba na kusafirisha ufuta kwenda nje ya nchi kupitia bandari ya Dar es Salaam alafu wakulima wa zao hilo wakiendelea kuwa masikini.

""Juzi nilikuwa Dar es Salaam, nimejionea Meli zikisafirisha shehena za ufuta kwenda nje leo mnaozalisha mnabaki kuwa masikini."" 

Nae Denis Kasonso mkulima  kutoka kata ya Kamsamba amesema anaungana na Ntila kuhusu uundwaji wa Sungusungu kwani tegemeo la mkulima ni mazao na mifugo, kitendo cha kuwaibia kinawarudisha nyuma kiuchumi.

"Mkulima anaendesha maisha yaje na familia  anasomesha na kufanya kila jambo akitegemea kilimo na ufugaji,kitendo cha kumuibia mazao au mifugo kutamfanya adidimie kiuchumi na kushindwa kuendesha familia hivyo ulinzi shirikishi una takiwa " amesema.

Comments

Popular posts from this blog

KAEGELE NA KAZUKAMWE WAIBUKA KIDEDEA KURA ZA MAONI CCM WILAYANI NKASI

DIWANI KATA YA KALA AFARIKI DUNIA KWA UGONJWA WA KIHARUSI

Mke wa Mchungaji wa kanisa la EAGT ajinyonga akihofia deni lake la fedha za kanisa