Tozo za chanjo za mifugo zazua balaa Songwe
Na Ibrahim Yassin,Songwe
WANANCHI jamii ya wafugaji kutoka bonde la Kamsamba wilayani Momba mkoani Songwe wamezikusanya risiti walizopewa baada ya kutozwa tozo za chanjo ya mifugo zilizoandikwa majina ya mikoa ya Katavi na Kigoma jiji huku wakitaka ufafanuzi.
Wananchi hao jana wamekusanya risiti hizo na kuzikabidhi kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na mdau wa maendeleo na mkulima bora wa bonde hilo Abdul Ntila uliolenga kutoa elinu ya uelewa kwa wakulima kupinga wanasiasa kugeuka daraja la kuwanyonya kupitia stakabadhi gharani kwa zao la ufuta.
Awali akizungumza kwenye mkutano huo Sakala Sinkala mkazi wa Mpapa alisema wapo kwenye zoezi la kuchanja mifugo yao na wanapolipa fedha wanapewa risiti zenye majina ya mkoa wa Katavi na Kigoma jiji hivyo wanaomba sababu kwani ni bora ziandikwe jina la Momba ama mkoa wa Songwe.
Nae Samwel Silumbwe mkazi wa Mkonko alisema katika bonde hilo kuna wafugaji wengi, kima cha chini kaya moja inakuwa na ng"ombe 200 na wao wamekubali kuchanja lakini wanamashaka kama halmashauri inapigwa kutokana na risiti kusoma mikoa mingine.
" Ndugu Adbul Ntila, sisi ni wafugaji pia ni wakulima wakubwa wa ufuta, Mtama, Mahindi na mazao mengine, tumekubali kuunda umoja ili kuhepuk a baadhi ya wanasiasa wanaotumia kivuli cha stakabadhi gharani kutudalalia,lakini pokea risiti hizi waone wahusika tupate majibu" alisema.
Akijibu maombi hayo Abdul Ntila Mkulima bora na mdau wa maendeleo ambaye siku za hivi karibuni alitoa 200.000 kusaidia ujenzi jengo la kujifungulia kijiji cha Mpapa na alitoa fedha zingine kuhani msiba kijijini humo alisema majibu sahihi yatapati kana atawasilina na viongozi kujua ukweli.
" Ndugu wananchi, leo nimekuja na waandishi wa habari ili mambo yawe wazi, ujio wangu ni kuhamasisha kuunda umoja wa wakulima na kuunda vikosi vya sungusungu ili mazao na mifugo yao iwe salama baada ya kuibuka wizi licha ya suala la risiti kuibuka "amesema.
Alisema risiti zilizokusanywa hapa mezani zimeandikwa Katavi na kigoma na kwamba ufafanuzi wa jambo hili utapatikana kupitia viongozi husika kama kuna upigaji wa hela itajulikana na kuwataka wawe watulivu.
Afisa mifugo wilayani Momba Tito Eleuter Ndegela alikiri risiti hizo kutumika na kudai ni takwa la mzabuni aliyepewa tenda ya chanjo kwani baada ya kuibuka homa ya Kimeta wizara iliamua kutumia mzabuni kuendesha zoezi hilo hivyo anaweza kutumia risiti.
Alisema serikali kupitia wizara ilianzisha utaratibu huo kutibu mifugo kupitia mdhabuni mwenye kampuni ambapo Momba wanamzabuni kampuni ya LEMAS RANGING & AGROVET CO LTD yenye makao makuu Sumbawanga mkoa wa Rukwa na analipa halmashauri asilimia 0.03 ya pato analopata kupitia tozo ya chanjo hizo.
Aliongeza kuwa kama mzabuni kapewa tenda anauwezo wa kutumia risiti za kampuni yake hiyo sio mbaya ila inabidi wananchi wapatiwe elimu wasione kama wanaibiwa.
Alisema baada ya ugonjwa wa kimeta kuibuka wameamua kuichanja mifugo yote kupitia makampuni yanayotoa risiti zao wao wakichukua asilimia 0.03 ya mapato ghafi ili kuondoa maambukizi hayo licha ya kuwa wapo watu waliokumbwa na maambukizi hayo.
Alisema Zahanati ya Chuo,Kahongo na Usiche ni miongoni mwa zahanati zilizokuwa na wagonjwa wa kimeta ambapo Mwezi October 2022 ndani ya mwezi mmoja pekee wagonjwa 125 waligunduli ka kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
Alisema Mwaka 2023 walitoa elimu kwa wananchi na kuendesha zoezi la chanjo ambapo watu 16 waliambukizwa na mwaka 2024 katika vijiji vya Kasano,Mpapa na Kahongo,watu 6 pekee ndiyo walioambukizwa kutoka Chitete na Naming'ng' na kwamba idadi imepungua kwa sababu ya utoaji elimu.
Aliongeza kuwa kama kuna malalamiko hayo timu ya wataalam itapita bonde zima la Kamsamba hilo kuwaelimisha wananchi jamii ya wafugaji kuhusu risiti hizo ili kuondoa sintofahamu iliyopo.



Comments
Post a Comment