Nanyaro atoa msaada wa Vifaa na kuwalipia bima Wanafunzi Kamsamba
Na Ibrahim Yassin.Songwe
Mjumbe wa halmashauri kuu ya chama cha mapinduzi mkoa wa Songwe Ombeni Nanyaro ametoa computer 5 na printer 2 zikiwa na thamani ya Milioni 5 kwa ajili ya wanafunzi kujifunza masuala ya computer wawapo shuleni.
Akiwa na viongozi wa Chama hicho, walimu, wanafunzi na baadhi ya wazazi Jana alikabidhi vifaa hivyo ili wanafunzi katika shule hiyo inayo milikiwa na jumuiya ya wazazi (CCM) waweze kujifunza masomo ya Computer.
Aidha Nanyaro alitoa Tsh, 500.000 na kuanzisha harambee ya kuchangisha fedha kwa viongozi wengine waliofika shuleni hapo na kupatikana Tsh, Milioni 2.5 zitakazotumika kujenga bweni la wavulana.
Bweni hilo litakuwa ni la pili baada ya siku za hivi karibuni kutoa fedha zake kulikarabati bweni chakavu la wasichana na kuweka miundombinu rafiki na kuvuta maji safi na salama kunusuru wanafunzi kutembea umbali mrefu kusaka maji.
Mbali na misaada hiyo Ombeni ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya Shule hiyo amemuagiza mkuu wa Shule hiyo Mwl, Howa kumpa idadi ya Wanafunzi ili awakatie bima za afya wawe wanatibiwa bure.
"Mkuu wa shule utanipa idadi ya wanafunzi watakaojiunga ili niwakatie bima itakayowafanya wazazi kuwa na amani ya moyo na kwa sasa fanyeni mazungumzo na wazazi kupitia vikao kuhakikisha kila mtu anapata taarifa hii"alisema.
Mwl.Howa ni mkuu wa shule hiyo licha ya kumpongeza mdau huyo alisema kwa sasa shule hiyo inang'ara huku akiwa na uhakika wa kuongezeka ufauru mara dufu.
"Mdau huyu mungu ampe maisha marefu' awali alivuta maji safi na kujenga jiko la kisasa kwa Tsh 700.000 na pia akatoa Tsh, Milioni 2.5 kukarabati bweni na sasa amewezesha Milioni 2.5 zitakazo jenga bweni la wavulana na ametoa Computer na Printer za Milioni 5.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake Anastazia Mwashitete alisema maboresho ya shule hiyo yamewaongezea hamasa ya kusoma hivyo wanamuahidi mdau huyo ufaulu mzuri wa alama A.
Shule ya sekondari Kamsamba ni moja ya shule kongwe wilayani Momba inayomilikiwa na jumuiya ya wazazi wa chama cha mapinduzi ilikuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi ambazo zimeondolewa na kuwa kivutio.



Comments
Post a Comment