Mwenyekiti serikali ya Mtaa auawa kikatili akutwa kwenye ukuta wa shule




Na Ibrahim Yassin.Songwe

ALIYEKUWA mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Hewe kijiji cha Itepula wilayani Mbozi mkoani Songwe, Jamson Mwakitalima Mtafya (59) amekutwa ameuawa kisha mwili wake kutupwa kwenye ukuta wa shule ya msingi Ndyuda akitokea benki kutoa fedha.

Akizungumza leo August 22/2024 jirani wa marehemu huyo, Assa Kamwela alisema marehemu jana aliaga nyumbani kwake kuwa anaenda benki kutoa hela majira ya asubuhi lakini hakurudi hadi majira ya mchana alipokutwa pembezoni mwa ukuta wa shule ya msingi Nyuda akiwa amekufa.

Alisema marehemu hakuwa na ugomvi na mtu kwani aliwahi kuwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa miaka 5 iliyopita na alikuwa mshauri mzuri kwenye jamii katika masuala mbalimbali.



Mwenyekiti wa kijiji cha Itepula Bonifasi Mkisi alisema marehemu alitoka nyumbani kwake jana saa moja asubuhi kwenda Mlowo kutoa fedha akiwa na usafiri wa pikipiki lakini siku hiyo hakurudi hadi walipomkuta kauawa na kutupwa kwenye uzio wa shule ya Ndyuda.

Alisema tukio hilo ni muendelezo wa matukio katika kijiji na kata ya Itaka kwa ujumla hivyo analiomba jeshi la polisi kuongeza kasi ya operesheni kukomesha vitendo hivyo.

Mwenyekiti huyo alipongeza kuwa kipindi hiki ni cha mavuno, watu wamelima wanauza mazao wanapoenda benki wanakuwa wanaviziwa na wezi na kuhatarisha maisha yao.



"Nilipigiwa simu kuelezwa uwepo wa tukio hili lilipofika eneo la tukio nikaukuta mwili huo ndipo nilipopiga simu polisi ambao walifika haraka na kuuchukua mwili huo na kuondoka nao hivyo kama.kijiji tunaendelea na taratibu zetu kubaini wahusika" alisema.

Kamanda wa Polisi mkoani Songwe, Augustino Senga, licha ya kukiri uwepo wa tukio hilo alisema walifika eneo la tukio majira ya saa 7 mchana na kuukuta mwili ukiwa na michubuko shingoni huku damu ikitoka puani.

Alisema uchunguzi wa awali imebainika kuwa mtu huyo aliuawa sehemu nyingine na akatupwa pembezoni mwa shule ya msingi Ndyuda na mwili huo umechukuliwa na kutunzwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti baada ya uchunguzi wa kitabibu kukamilika.

Aliongeza kuwa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kufuatia tukio hilo huku uchunguzi wa kuwabaini wahusika unaendelea na watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kuwapeleka mahakamani pindi watakapo wakamata.

Kamanda Senga alitoa rai kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kufanya mauaji na hata kama kuna jambo mtu kafanyiwa ni bora aende kwenye vyombo vya kisheria ili haki yake ipatikane kuliko kutoa uhai wa mtu.



"Rai yangu kama una jambo ni bora uende kwenye vyombo vya kisheria na si kufanya mauaji kama kulipiza kisasi kwani kufanya hivyo ni sawa na uharifu wa mauaji vyombo vya sheria vipo tuvitumie kutatua chaangamoto zilizopo"alisema kamanda Senga.

Baadhi ya watu walitoa maoni mbalimbali kufuatia tukio hilo huku wengine wakidai marehemu huyo baada ya kutoa hela benki kuna watu walimnyemelea na kumpora fedha kisha kumuua licha ya kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa jam bo hilo.

Comments

Popular posts from this blog

KAEGELE NA KAZUKAMWE WAIBUKA KIDEDEA KURA ZA MAONI CCM WILAYANI NKASI

DIWANI KATA YA KALA AFARIKI DUNIA KWA UGONJWA WA KIHARUSI

Mke wa Mchungaji wa kanisa la EAGT ajinyonga akihofia deni lake la fedha za kanisa