DC ITUNDA AKUTANA NA UONGOZI WA KAMPUNI YA MAMBA INAYOWEKEZA KWENYE UCHIMBAJI WA MADINI ADIMU DUNIANI RARE EARTH METALS ENEO LA NGWALA.
Na Ibrahim Yassin.Songwe
Mkuu wa Wilaya ya Songwe Solomon Itunda jana amefanya kikao na uongozi wa Kampuni ya Mamba Minerals inayowekeza katika uchimbaji wa madini adimu duniani ya Rare Earth Metals kijiji cha Ngwala Wilayani Songwe.
Kikao hicho ambacho pia kimehudhuriwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Songwe, Godfrey Kawacha kimefanyika katika ofisi za Mkuu wa Wilaya zilizopo Mkwajuni makao makuu ya wilaya.
Akizungumza baada ya Kikao hicho, Mhe. Itunda amesema kuwa uongozi huo umemweleza maendeleo ya mchakato wa tathmini na mipango ya kuanza kulipa fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yalichukuliwa kupisha mradi.
Mkuu huyo wa Wilaya ameusisitiza uongozi huo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa kila hatua wanayofikia ili wananchi wajue kinachoendelea katika eneo hilo.
Pia, DC Itunda amesema kuwa uongozi huo umemweleza kuwa ujenzi wa mgodi huo utaanza Januari, 2025.
"Tumefanya kikao na wenzetu wa Mamba, Kampuni ambayo inayowekeza katika uchimbaji wa madini adimu duniani ya Rare Earth Metals kule Ngwala. Kampuni hii wanaanza ujenzi wa vyumba vya madarasa shule ya sekondary Ngwala na Kituo cha Polisi kule Ngwala" amesema DC Itunda.
Wawakilishi wa Kampuni hiyo wameongozwa na Mkurugenzi wa Mamba Minerals Corporation Limited ( MML), Ismail Diwani ambae amemhakikishia mkuu huyo wa wilaya kuwa kila kitu kitakwenda sawa .
Diwani amesema kuwa ujenzi wa mgodi huo utaanza Januari, 2025 na kuhusu ujenzi wa kituo cha polisi na shule ya sekondari Ngwala utaanza siku za hivi karibuni
Amsema nia na dhamira ya kujenga kituo hicho ni kuhakikisha hali ya ulinzi inakuwepo muda wote kwani hilo ni eneo la uchimbaji huku shule itakayojengwa itasaidia watoto kusoma karibu na makazi yao.



Comments
Post a Comment