Wenyeviti wa vijiji wapewa wiki mbili kuwasomea Wananchi Mapato na matumizi
Na Israel Mwaisaka,Rukwa
MKUU wa wilaya Nkasi Peter Lijualikali ametoa wiki mbili toka sasa kwa viongozi wa vijiji kuhakikisha kuwa wanaitisha mikutano mikuu ya vijiji na kuwasomea Wananchi mapato na matumizi kabla ya kuufikia uchaguzi wa serikali za mitaa mwishoni mwaka huu.
Agizo hilo amelitoa jana kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ambapo ameda kuwa ni lazima wenyeviti wa vijiji na watendaji wa vijiji kuhakikisha wanawasomea Wananchi mapato na matumizi ya vijiji vyao ili wananchi weweze kujua maendeleo ya vijiji vyao.
Hivyo amewaagiza Maafisa tarafa na watendaji wa kata kuhakikisha katika maeneo yao wanayoyaongoza wenyeviti wote wa vijiji wawe wameitisha mikutano mikuu ya vijiji na kuwasomea wananchi mapato na matumizi.
Alidai kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi ni vyema kabla ya kuingia kwenye uchaguzi Wananchi wakayajua mapato yao ikiwa ni pamoja na kujua mipango endelevu ya Kijiji chao na kutokufanya hivyo kutawaacha Wananchi na sintofahamu lakini pia hata mwenyekiti mpya kama atapatikana atakua hajui wapi pa kuanzia ikiwa ni pamoja na wananchi wenyewe
“Wenyeviti wengi hawawasomei wananchi wao mapato na matumizi na wengi wao wamekua wakiogopa kuitisha mikutano hiyo ya vijiji na sijui ni kwa nini hili linajitokeza lakini sasa nawapeni wiki mbili hizi tekelezeni kwa vitendo na Maafisa tarafa na watendaji wa kata hakikisheni hili linatekelezeka katika maeneop yenu”alisema
Pia mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Nkasi Pankrasi Maliyatabu amewataka Watendaji wa vijiji kuendelea kukusanya mapato katika maeneo yao kwani hiyo ni moja ya kazi yao kubwa katika ajira zao.
Amesema kuwa kuna baadhi ya maeneo Watendaji wa vijiji hawaifanyi kazi hiyo na kuwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na kanuni za ajira zao na kuwa sasa hataki tena kusikia jambo hilo
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa wilaya Mayuma Zilantuzu amedai kuwa wamepokea hoja nyingi kutoka kwa Madiwani pamoja na viongozi na kuwa zile hoja ambazo inabidi zifanyiwe kazi watazitekeleza kwa wakati na kubwa ni kutaka kuwaletea Wananchi maendeleo



Comments
Post a Comment