JMAT- VIONGOZI WA DINI WASIKUBALI KUTUMIWA NA WANASIASA


Na Israel Mwaisaka,Rukwa

VIONGOZI wa Dini wilayani Nkasi mkoani Rukwa wametakiwa kusimama imara na kutoruhusu kuyumbishwa na Wanasiasa katika kipindi hiki tunachoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.

Wito huo umetolewa leo na mwenyekiti wa jumuia ya maridhiano na amani Tanzania (JMAT) wilaya Nkasi Hadhiri Daruweshi alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha jumuia hiyo ambapo amedai kuwa viongozi wa dini wakiyumba wanaweza kuwatoa nje ya mstari waumini wao na kubaki na sintofahamu.

Amesema kuwa wao kama viongozi wa dini jukumu lao kubwa katika kipindi hiki kuelekea katika chaguzi hizo kubwa ni kujikita zaidi katika kuhubiri amani na upendo kwa nguvu zote kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kuwepo kwa amani katika taifa hili.

Hadhiri amedai kuwa kwa uzoefu katika maeneo mbalimbali duniani ambako viongozi wa dini wamechanganya siasa na dini ni lazima kuwepo kwa machafuko na kunakotokana na kutoweka kwa amani katika  jamii hiyo.

Awali katibu wa jumuia hiyo Mchungaji Fidelis Maheke alidai kuwa kazi ya viongozi wa dini ni kumtangaza Mungu na Amani pamoja na maisha bora kwa waumini wao na kukemea vitendo vya baadhi yao viongozi wa dini kutumika na Wanasiasa

Alidai kuwa viongozi wa dini wanayo dhamana kubwa kutoka kwa watu wanaowaongoza na kuwa heshima waliyonayo wasiitumie vibaya kwa kuwachanganya Waumini wao na mambo ya kisiasa na wala wasikubali kuwa wapiga debe wa wanasiasa.

Mwinyi Abdallah Jumbe mmoja wa wajumbe wa JMAT naye aliwataka viongozi wenzie kusimamia maandiko kama yalivyoandikwa kwenye vitabu vitakatifu na kuwa kwenda kinyume na maadili kwa kufanya mambo kinyume na hayo ni kumkosea Mungu na watu anaowaongoza.

Mmoja wa wadau wa kikao hicho Salumu Kazukamwe aliwataka viongozi hao wa dini kujitahidi kusimamia maadili ya kazi yao kwani viongozi wa dini ni watu muhimu sana katika msitakhabari wa kuhakikisha amani inatamalaki Nchini katika kipindi chote.

Alisema kuwa wao kama viongozi wa dini wanategemewa sana na waumini wao hivyo wanatakiwa kusimamia maadili yao ya kazi kwani kubwa walilonalo ni kuwahubiria Watu juu ya kumjua Mungu sambamba na kufundisha maadili yaliyo mema.

Kazukamwe alidai kuwa kama wanasiasa watakua na nguvu na ushawishi kwa viongozi wa dini na kutuutumia ushawishi wao na kuanza kuwatumia viongozi wa dini amesema kuwa taifa litakwenda pabaya bali wawe na msimamo na wajikite katika kuutangaza ufalme wa Mungu .



Comments

Popular posts from this blog

KAEGELE NA KAZUKAMWE WAIBUKA KIDEDEA KURA ZA MAONI CCM WILAYANI NKASI

DIWANI KATA YA KALA AFARIKI DUNIA KWA UGONJWA WA KIHARUSI

Mke wa Mchungaji wa kanisa la EAGT ajinyonga akihofia deni lake la fedha za kanisa