MCHAKATO WA KUPUMZISHA ZIWA TANGANYIKA WAKAMILIKA VIONGOZI WAPIGWA MSASA
Na Israel Mwaisaka,Nkasi
KAIMU mkuu wa wilaya Nkasi ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Kalambo Razaro Komba amewataka Madiwani,Viongozi wa vijiji na watumishi wote wa serikali kuhakikisha kuwa wanatoa elimu kwa wananchi katika maeneo yao juu ya hadhima ya serikali ya kutaka kulipumzisha ziwa Tanganyika kwa muda wa miezi mitatu
Akizungumza kwenye kikao kilichowakutanisha madiwani na viongozi wa vijiji vilivyo katika mwambao wa ziwa Tanganyika na timu ya wataalamu kutoka wizara ya mifugo na Uvuvi amesema kuwa lengo la serikali ni kutaka kulipumzisha ziwa hilo ili kuwapa muda samaki kuweza kuzaliana na kuongeza kipato cha Wavuvi kuweza kuvua samaki wengi na wakubwa wanaostahili.
Amedai kuwa kinachotakiwa ni wananchi kuuelewa mpango huo vizuri na kujua faida zitakazopatikana baada ya ziwa Tanganyika kupumzishwa kwa kipindi hicho cha miezi mitatu ikiwa ni pamoja na kila mmoja kuwa mlinzi kwa mwenzie katika kuhakikisha katika kipindi hicho cha miezi mitatu hakuna mtu atakaeingia ndani ya ziwa na kufanya shughuli ya uvuvi
Sambamba na hilo ameiomba wizara ya Uvuvi na mifugo kuongeza vikundi vya uvuvi (BMU) kwani uzoefu unaonyesha kuwa katika maeneo ambayo BMU zimeanzishwa kuna ufanisi mkubwa na wamekuwa walinzi wakubwa kwa wenzao wanaokwenda kinyume na ametamani zoezi hilo lingefanyika hata kabla ya Mei 15 ziwa hilo litakapopumzishwa.
Mteknolojia wa Samaki kutoka wizarani Masui Munda amedai kuwa mpango wa kulipumzisha ziwa Tanganyika umetokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa na kuona kuwa ziwa Tanganyika Samaki wameendelea kupungua kwa kasi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uvuvi haramu na kuharibu mazalia ya samaki na suluhisho pekee ni kulipumzisha ziwa hilo ili kuwapa samaki nafasi ya kuzaliana.
Alisema kuwa wao kama wizara walienda mbali zaidi kwa kushirikiana na Nchi tatu zinazolitumia ziwa Tanganyika ambazo ni Zambia,DR –Congo na Burundi na kuweka azimio la pamoja ambapo nchi zote itapofika Mei 15 zitalifunga ziwa hilo na kufanya doria ya pamoja ya kukabiliana na Wavuvi ambao watashindwa kutekeleza agizo hilo la serikali.
Imelda Adamu mwakilishi wa mkurugenzi wa Uvuvi na kaimu mkurugenzi wa tafiti na mafuzo ya uvuvi na afisa uvuvi mkuu Owen Kibona wamesema kuwa kama zoezi hili litakwenda vizuri Wananchi wenyewe watayaona matokeo baada ya ziwa hilo kufunguliwa baada ya kupumzishwa kwa kipindi hicho cha miezi 3 kwa maana mavuno ya samaki yataongezeka na kuongeza kipato chao katika ngazi ya familia na pato la taifa
Madiwani kwa upande wao waliitaka serikali kuhakikisha katika kipindi hicho wanawadhibiti watendaji wa idara ya uvuvi ili wasutumie muda huo kujinufaisha kwa kuwaruhusu watu wachache wafanye uvuvi na kuomba kuwepo na kikosi maalumu cha doria kuweza kuwadhibiti wavuvi watakaokaidi agizo hilo
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Nkasi Pankrasi Maliyatabu amesema kwamba kama viongozi wa vijiji na Madiwani watatekeleza wajibu wao sawasawa wa kuielimisha jamii juu ya mpango huo wa serikali wa kulipumzisha ziwa anaamini jambo hilo litakelezeka vizuri kwa maana Wananchi wengi wa sasa wanao uelewa mkubwa wa mambo lakini pia na wao wanaona hari ya uvuvi ilivyo dorora na samaki wanaovuliwa ni wadogo hivyo ni lazima watakubaliana na mpango huo mzuri wa serikali




Comments
Post a Comment