Mbaroni kwa ubakaji na mauaji ya Mwanamke
Na Israel Mwaisaka,Rukwa
Polisi mkoani Rukwa inamshikilia Daudi Mwanalinze (25) akituhumiwa kumbaka na kumsababishia kifo Martha Zacharia (32) .
Mtuhumiwa huyo wa mauaji na marehemu ni wakazi wa eneo la Makutano lililopo nje kidogo ya Mji wa Sumbawanga.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa,Shadrack Masija amethibithisha kutokea ka tukio hilo wakati akizungumza na wanahabari jana ofisini kwake mjini Sumbawanga.
Akizungumzia hilo alisema mwili wa Martha ulikutwa Februari, 02mwaka huu asubuhi katika eneo la Makutano nje kidogo ya Mji wa Sumbawanga.
" Mwili wa marehemu ulifanyiwa ukaguzi wa kitabibu katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga na matokeo yake yalionesha kuwa alibakwa au kuingiliwa kimwili" alieleza.
Aliongeza kuwa Polisi kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo wa mauaji Machi 06, mwaka huu mkoani Kigoma alikokuwa amejificha.
" Tumemkamata mtuhumiwa wa mauaji (Daud) Machi,06 mwaka huu huko mkoani Kigoma alikokuwa amekimbilia kujificha. Kwa sasa tunakamilisha taratibu za kumfikisha mahakamani" alieleza.
Aliwashukuru wananchi waliokuwa bega kwa bega na Jeshi la Polisi kutoa taarifa zilizowezesha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.
Aidha aliwataka wananchi wanaochukia uhalifu wasichoke kutoa taarifa kwa jeshi hilo.
"Niwatake wananchi wasijihusishe na uhalifu wa aina yoyote kwani kamwe haulipi. Hata ukijificha popote pale tutakukamata tu" alisisiza
Mwisho.

Comments
Post a Comment