Mzazi awamotisha Walimu baada ya shule kufanya vizuri kwenye matokeo ya darasa la saba



Na Israel Mwaisaka,Rukwa

MMOJA ya Wazazi wa watoto wanaosoma shule ya msingi Kipundukala kata ya Namanyere wilayani Nkasi mkoani Rukwa ametoa motisha kwa Walimu wa shule hiyo kwa kuwanunulia vitenge doti 8 baada ya shule hiyo kufanya vizuri kwenye mtihani wa darasa la saba baada ya kushika nafasi ya saba kiwilaya na tisa kimkoa.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhiwa zawadi hiyo ya vitenge leo mwalimku mkuu wa shule hiyo Josephat Labani aliwaeleza walimu wa shule hiyo kuwa mmoja wa wazazi wa Watoto wanaosoma katika shule hiyo Issa Kabuje ametoa zawadi ya vitenge kwa walimu wa shule hiyo kama Motisha kwao kutokana na maendeleo mazuri kwa shule hjiyo kuendelea kupandisha ufaulu kwa kila mwaka.


Alidai kuwa vitenge hivyo vimekabidhiwa ofisini kwake siku chache zilizopita na kuwa leo ni siku muhimu ya kukabidhiwa kila mwalimu zawadi yake ya kitenge iliyotolewa na mzazi huyo baada ya kuitambua kazi nzuri inayofanywa na walimu.

Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Angelina Mwampashi amempongeza mzazi huyo kwa hicho alichokifanya na kuwa mzazi huyo ameacha deni kwao la kuhakikisha Walimu wanaendelea kufundisha kwa moyo na kuwa kitendo hicho kilichofanywa na mzazi huyo kama kitafanywa na watu wengine kitaendelea kuwatia moyo Waalimu ya kufundisha kwa nguvu na moyo na kupata matokeo mazuri zaidi.

Alisema kuwa yeye kama kiongozi wa kamati ya shule atakachokifanya ni kujenga mshikamano uliopo kati ya wazazi na Walimu na kubwa ni kuona kiwango cha taaluma kinapanda kama walivyofanya sasa na kuwa hawapo tayari kumuona mwalimu atakayewarudisha nyuma katika mikakati waliyojiwekea ya kukuza taaluma.

Afisa elimu wa kata hiyo ya Namanyere Kasilida Milala amedai kuwa mzazi huyo ni mmoja ya watu waliofanya mabadiliko ya kifikra kwa kuwapongeza waalimu pale walipofanya vizuri na kuwataka wazazi kujenga ukaribu na walimu badala ya kutengeneza uadui kati yao na kuwa kitendo cha Issa Kabuje kutoa zawadi hiyo kimewatia nguvu walimu kuendelea kufundisha zaidi tena kwa moyo.

Akizungumza na Waandishi wa habari Kabuje amedai kuwa vitenge hivyo vina thamani ya zaidi ya shilingi laki tatu na kuwa yeye ameamua kufanya hivyo baada ya kuona jitihada zinazofanywa na walimu wa shule hiyo katika kuinua taaluma.


Alifafanua kuwa Walimu wanafanya kazi kubwa kama sehemu ya Walezi wa Watoto wao na kuwa muda mwingi Watoto hao wanaishi na Walimu hivyo ipo sababu ya kuwamotisha kwa namna yoyote inayowezekana.



Comments

Popular posts from this blog

KAEGELE NA KAZUKAMWE WAIBUKA KIDEDEA KURA ZA MAONI CCM WILAYANI NKASI

DIWANI KATA YA KALA AFARIKI DUNIA KWA UGONJWA WA KIHARUSI

Mke wa Mchungaji wa kanisa la EAGT ajinyonga akihofia deni lake la fedha za kanisa