Mtandao wa Polisi Wanawake TPF-NET Nkasi watoa msaada kwa Wazee kuelekea maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani


Na Israel Mwaisaka,Nkasi
KATIKA kuelekea maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika Marchi 8 ya mwaka huu mtandao wa Polisi Wanawake TPF-NET wilayani Nkasi mkoani Rukwa wametoa msaada wa vitu mbalimbali vya matumizi ya nyumbani kwa Wazee vyenye thamani ya zaidi ya laki tano.

Akikabidhi vitu hivyo kwa Wazee hao Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake wa wilaya Mkaguzi msaidizi wa Polisi Ivona Mwanga amesema wao kama polisi wanawake wanautambua mchango wa Wazee katika taifa hilo na ndiyo maana wameamua kuwaona na kuwapatia baadhi ya vitu kama sehemu ya utambuzi wa mchango wao mkubwa kwa taifa.

Alisema kuwa siku ya Wanawake Duniani imelenga kutambua mchango wa Wanawake katika jamii na kubwa ndani ya jeshi la Polisi ni kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa kuweka usawa katika mizania ya haki kwani kila mmoja ana haki ya kuishi bila kubughudhiwa bila kujali jinsi yake.


Mwanga amedai kuwa Wazee ni moja ya kundi muhimu ambalo limepigania haki mbalimbali ikiwemo na za Wanawake na Watoto kiasi cha sasa kila mmoja angalau anaheshimika kwa nafasi yake bila ya kujali jinsia na kuwa hayo ni maendeleo makubwa.

Mwenyekiti wa dawati la jinsia Anna Kisimba amesema kuwa Dawati la jinsia ni zao la mtandao huo wa Polisi Wanawake na kuwa kwa kuzingatia kauli yao ya ‘Uzee na Kuzeeka havikwepeki ndiyo maana wakatoa kipaumbele kwa Wazee katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani na kuwa wao kama jeshi la Polisi bado wanahitaji busara toka kwa Wazee katika kufanikisha suala la usawa katika jamii.


Na akawataka Wazee kuendelea kuyasimamia maadili mema katika jamii ikiwa ni pamoja na kukemea vitendo mbalimbali vya kikatili dhidi ya Wanawake na kuwa kama wazee watashiriki ipasavyo katika vita hiyo kuna uwezekano mkubwa vitendo vya ukatili wa aina yoyote vitatoweka kabisa katika jamii.

Mwenyekiti wa jukwaa la Wanawake wa mkoa Rukwa Suzana Ndotela kwa upande wake ameomba Wazee kuendelea kuwasimamia vijana weao na kutoa ushirikiano katika kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na kuwa mpaka hapa taifa lilipofikia kiasi cha vitendo hivyo viovu kupungua Wazee wanao mchango mkubwa katika hilo


Afisa maendeleo ya jamii Farida Nyang’uye amewashukuru Polisi Wanawake kwa kuwatambua Wazee katika vita hiyo ya kuelekea usawa kati ya Wanawake na jinsia nyingine ya kiume kwani wote wana haki sawa katika jamii na kila mmoja anatakiwa kutekelezewa haki zote za msingi bila ya kubaguliwa kwa namna yoyote.

Mwenyekiti wa mtandao wa Wazee wilaya Nkasi kupitia shirika lisilo kuwa la kiserikali la NKANGO Jeneroza Kayanda (Mama Kadenge) amewashukuru Polisi kupitia mtandao wao wa Polisi Wanawake kwa kuwatambua Wazee kama sehemu ya jamii katika mapambano ya kutafuta usawa wa kijinsia na kuwa wao kama Wazee watatoa ushirikiano wa kutosha kwa jeshi hilo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanaishirikisha Watoto wao katika kuwaeleza umuhimu wa usawa wa kijinsia katika jamii.

Vitu vilivyotolewa kwa Wazee hao ni mifuko ya sukari,Katoni za sabuni za mche na unga,Chumvi,Mafuta na vinginevyo vyenye thamani ya zaidi ya Tshs,500,000

Comments

Popular posts from this blog

KAEGELE NA KAZUKAMWE WAIBUKA KIDEDEA KURA ZA MAONI CCM WILAYANI NKASI

DIWANI KATA YA KALA AFARIKI DUNIA KWA UGONJWA WA KIHARUSI

Mke wa Mchungaji wa kanisa la EAGT ajinyonga akihofia deni lake la fedha za kanisa