Ajeruhiwa na Tembo akienda shambani
Na Israel Mwaisaka,Nkasi
KIJANA mmoja aliyefahamika kwa jina la Shija Machenga (19) mkazi wa kijiji cha Itete kata ya Itete wilayani Nkasi mkoani Rukwa amejeruhiwa vibaya baada ya kukanyagwa na Tembo.
Akizungumzia tukio hilo afisa mtendaji wa kata ya Itete Justin Mangazini amesema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa 2 za asubuhi wakati kijana huyo alipokuwa akielekea shambani.
Amesema kuwa kijana huyo alikua ameongozana na Mbwa wake watatu alipokuwa akielekea shambani na wakiwa njiani katika eneo la kitongoji cha Sokonso Mbwa walinusa harusu ya Tembo na kuanza kumfuata alipokuwa na ndipo alipoanza kuwafukuza Mbwa hao .
Katika jitihada za kujiokoa Mbwa hao dhidi ya Tembo walikimbilia alipokuwepo mwenye Mbwa pasipo yeye kujua na alipomuona Tembo akiwa karibu na yeye aliamua kuanza kukimbia ili kujiokoa lakini alianguka na ndipo Tembo huyo alipomkanyaga na kumjeruhi vibaya katika mguu wake ambapo nyama za mguuni zilinyofoka na kumsababishia maumivu makali.
Diwani wa kata ya Itete Galincha Kiliko alidai kuwa baada ya tukio hilo na majeraha makubwa aliyoyapata waliamua kumkimbiza katika hospitali ya wilaya Nkasi kwa ajili ya matibabu.
Mkuu wa wilaya Nkasi Peter Lijualikali amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa majeruhi amepewa rufaa kupelekwa katika hospitali ya rufaa ya kanda ya Mbeya kwa matibabu zaidi.
Alidai kuwa Tembo huyo baada ya kumjeruhi kijana huyo alirudi ndani ya hifadhi ya Lwafi na hakuna taarifa nyingene mbaya kuhusiana na Tembo huyo.
Hivyo amewataka Wananchi hasa waliopo karibu na hifadhi za Wanyama pori kuwa makini sana wakati wa utekelezaji wa majukumu yao katika kujilinda na Wanyama pori kwani maeneo hayo ni sehemu yao hivyo wanaweza wakajitokeza wakati wowote


Comments
Post a Comment