Mwanamke auawa kwa imani za kishirikina
Na Israel Mwaisaka,
Sumbawanga
MWANAMKE aliyefahamika kwa jina la Mwashi Salita (60) mkazi wa Kijiji cha Chombe wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa ameuawa kwa kukatwa mapanga kutokana na Imani za kishirikina.
Tukio hilo lilitokea Novemba 20 majira ya saa 1 za usiku ambapo watu wasio fahamika walimvamia mwanamke huyo nyumbani kwake na kisha kumkata mapanga na kukimbilia kusikojulikana.
Akitoa taarifa za tukio hilo jana Kamanda wa Polisi mkoani humo, Shadrack Masija alisema kuwa watu hao walikwenda nyumbani kwa marehemu wakiwa na silaha mbalimbali za jadi ambapo walipofika walimkuta akiwa na wajukuu wake kisha walimvamia na kuanza kumpiga.
"kabla ya watuhumiwa hao kumkata mapanga, walimpiga kichwani kwa kutumia kitu butu, kitendo kilichosababisha kuanguka chini na kushindwa kupata msaada kwa kua aliokua nao walikua ni watoto kisha wakamkata mapanga katika sehemu mbalimbali za mwili wake" alisema.
Baada ya kumkata mapanga walimsababishia majeraha makubwa yaliyovuja damu nyingi na kwa kua hakupata msaada wowote wa wakukimbizwa katika kituo cha afya kwaajili ya matibabu, hivyo kupelekea kifo chake muda mfupi baadaye.
Kamanda huyo wa polisi alisema kuwa baada ya polisi kuanza uchunguzi wa tukio hilo walifanikiwa kuwakamata watu watatu wanao tuhumiwa kuhusika na tukio hilo.
Alisema kuwa watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani wakati wowote mara baada ya upelelezi wa awali kukamilika ili wakajibu tuhuma zinazo wakabili.

Comments
Post a Comment