Serikali kuwalipa wakulima wa mahindi fedha zao Oktoba 30
- Get link
- X
- Other Apps
Na Israel Mwaisaka,Rukwa
KATIBU mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa Daniel Chongolo amewataka Wakulima waliouzia mahindi serikali kupitia NFRA wawe na subira kwani mchakato unaendelea na malipo yanaweza kufanyika Oktoba 30 ya mwaka huu.
Ameitoa ahadi hiyo jana katika kijiji cha Ntalamila kata ya Myula wilayani Nkasi alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara baada ya mbunge wa jimbo la Nkasi kusini Vicent Mbogo kumweleza Chongolo kuwa kilio cha watu wengi katika eneo hilo ni malipo ya mahindi waliyoiuzia serikali.
Mbunge katika maelezo yake alisema kuwa wakazi wa wilaya Nkasi ni Wakulima na maisha yao kwa asilimia kubwa yanategemea kilimo na kuwa kitendo cha wao kutolipwa fedha zao kwa wakati kinawaumiza na kushindwa kufanya maandalizi ya kilimo katika msimu ujao wa kilimo kwa kununua pembejeo kwa wakati.
Kufuatia hari hiyo katibu mkuu wa CCM taifa Daniel Chongolo alitoa ahadi kuwa ifikapo Oktoba 30 ya mwaka huu wakulima watakua wamelipwa fedha zao na kuwa hiyo ni kero kubwa ambayo serikali imekua ikiishughulikia kwa wakati.
Na aliagiza kuwa sasa maduka ya kuuza mbolea ya ruzuku yasambazwe hadi vijijini ambako kuna Wakulima badala ya maduka hayo kusalia mijini na kuwapa shida wakulima kufuata mbolea hizo umbali mrefu.
Pia aliwapongeza wakazi wa kata ya Myula na wilaya Nkasi kwa ujumla kwa kuutambua umuhimu wa elimu baada ya kubaini kuwa wazazi wanao mwamko mkubwa wa kuwapeleka shule Watoto wao na kuwa msimamo huo waendelee kuwa nao kwani elimu ndiyo msingi wa kila kitu.
Lakini pia alizizungumzia barabara za Wampembe,Nkana -Kala na ya King’ombe –Mpasa kuwa serikali imeendelea kuzifanyia kazi na ndiyo maana kuna mabadiliko makubwa sasa ukilinganisha na siku za nyuma na kuwa wataendelea kutenga fedha katika barabara hizo walau ziweze kufanana na barabara nyingine hapa Nchini
Katika ziara hiyo ya siku 4 aliyoianza mkoani Rukwa jana akiwa wilayani Nkasi aliweza kukagua ujenzi wa shule ya sekondari Paramawe,Bwawa la maji la Mfiri,alikutana na mabalozi kwenye shina namba 3 kipundu,ukaguzi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya,ujenzi wa shule ya msingi Ntalamila ikiwa ni pamoja na kuzungumza na Madiwani na watu wa makundi mbalimbali.
- Get link
- X
- Other Apps


Comments
Post a Comment