CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoani Rukwa kimewasimamisha uongozi viongozi wa chama hicho wanao tuhumiwa kukihujumu kwa kuwauzia kadi za Kieletroniki viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ili wazitumie katika mikakati yao ya kisiasa.
Akitoa taarifa hiyo mwishoni mwa wiki Jana, Katibu wa Itikadi na uenezi wa chama hicho, Godfrey Mwanisawa alisema viongozi hao walikua wakichukua kadi za wanachama na kumuuzia Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Rukwa, Sadrick Malila, maarufu kwa jina la Ikuwo ili atangaze kuwa wanachama hao wamehamia Chadema na wamerudisha kadi za CCM.
Amesema kuwa baadhi ya kadi hizo ni ya aliyekuwa mwana CCM mkongwe marehemu Chrisant Mzindakaya pia marehemu Zuberi Kauzeni ambaye alikua mwenyekiti wa Jumuia ya wazazi tawi la King'ombe Kata ya Majengo pamoja na kadi za Wanachama wengine ambao wamehama mkoani Rukwa.
Katibu Mwenezi huyo amesema kuwa baadhi ya viongozi hao wa CCM waliokuwa wakiuza kadi hizo ni Chriss Mwalwanda ambaye ni Katibu kata ya Majengo, Alexander Kasongo Katibu wa Siasa na uenezi kata ya Majengo pamoja na Paul Kawambula Katibu wa UVCCM kata ya Majengo ambao wamesimamishwa ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo.
"Siku ya Octoba 2 Mwenyekiti huyo wa Chadema mkoa wa Rukwa aliita vyombo vya habari na kuonesha kadi za kieletroniki za Wanachama wa CCM akidai kuwa wamerudisha kadi hizo na kujiunga na Chadema, kumbe baadhi yao walikua ni marehemu na wengine wamehama mkoa ambazo aliuziwa na viongozi hao wanao tuhumiwa" alisema Mwanisawa.
Alisema kuwa kwa kitendo hicho alichofanya Mwenyekiti wa Chadema si sawa kwani mwanachama anayetakiwa kurudisha kadi anapaswa akabidhi yeye mwenyewe katika ofisi ya chama anachohamia ama katika mkutano wa hadhara wa chama lakini kilicho fanyika ni Siasa chafu zisizo na tija katika nyakati hizi ambazo Wanachama wanauelewa mkubwa wa masuala ya kisiasa.
Aliongeza kuwa kutokana na maendeleo makubwa yaliyofanywa na serikali ya CCM hakuna mwanachama atakaye rudisha kadi yake kizembe hivyo Wanachama wa chama hicho mkoa wa Rukwa wanatakiwa kutulia washikamane na wawe na umoja kwani CCM ipo imara na haita tetereka kwa propaganda hizo chafu.
Kwa upande wake Katibu wa CCM wilaya ya Sumbawanga, Tabu Hussein alisema kuwa kwa kawaida kadi za Wanachama baada ya kutengeneza ngazi ya taifa zinatumwa kwa viongozi wa mkoa, nao wanazipeleka ngazi ya wilaya na wao huzikabidhi kwa viongozi wa Kata ndio hao viongozi waliokuwa wakimuuzia kiongozi huyo wa Chadema.
Amesema kuwa tayari chama hicho kimeanzisha uchunguzi kwa viongozi hao wasio waadilifu pia kitachukua hatua kupitia wanasheria wa chama kwa mwanasiasa huyo wa upinzania aliyekuwa akifanya siasa chafu na kamwe CCM wilaya haitavumilia kuona wanasiasa wakiharibu nia yake nzuri ya kushinda chaguzi zijazo.
Comments
Post a Comment