Kijana adaiwa kutekwa ndugu wahaha kumtafuta

Na Mwandishi wetu,Sumbawanga

WATU wasiojulikana wanadaiwa kumteka kijana anayefahamika kwa jina la Friday Mbalwa (33) mkazi wa kitongoji cha Chanji Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa na Kisha kutokomea naye kusikojulikana.

Kwamujibu wa mke wa kijana huyo Cecilia Saki, alisema kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Oktoba 19 akiwa amelala chumbani na mume wake ndipo watu wapatao watano walivunja mlango wa nyumba wanayoishi na kuingia chumbani huku wakiwa na bunduki na mapanga.

Alisema kuwa watu hao baada ya kuingia chumbani walimuamuru mwanamke huyo kujifunika shuka hadi usoni na kumuonya asipige kelele, kisha kumtaka Mbalwa ainuke kitandani na kuanza kumpiga.

Inaidawa kuwa wakati wakimpiga Mwanamke huyo alisikia moja wa watu hao akimweleza mume wake kwamba......"tunafanya kazi pamoja za fundi kujenga lakini wewe unatudhulumu hatuwezi kukubali lazima tumalizane" alisema.

Alisema kuwa baada ya watu hao kutembeza kichapo kwa Mbalwa waliondoka naye na kuelekea kusikojulikana na hajarudi nyumbani hapo hadi leo hii.

Cecilia ambaye amezaa watoto wanne na mume wake huyo, alidai siku iliyofuata alitoa taarifa kwa uongozi wa mtaa kisha polisi ambapo lilifunguliwa jarada namba SUM/RB/488823.

Kwa upande wake, Baba mzazi wa kijana huyo, Felician Mwanambalwa aliliomba Jeshi la polisi kufanya uchunguzi ili kubaini alipo kijana wake kama yupo hai au amefariki dunia.

"Tunamuomba Mungu asaidie kijana wetu apatikane iwe mzima au amekufa maana sasa hatujui lolote" alisisitiza

Naye, Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Shadrack Masija akihojiwa alisema hana taarifa kuhusu tukio hilo lakini kama tayari limeripotiwa polisi watashirikiana na ndugu kuhakikisha wanapata taarifa za mtu huyo yupo hai au la.

"Mimi ndio nakusikia wewe, sina taarifa kabisa kuhusu tukio hili lakini naomba ndugu zake waje ofisini kwangu tupange mikakati ya kumtafuta kwa pamoja" alisema Kamanda huyo.



Comments

Popular posts from this blog

KAEGELE NA KAZUKAMWE WAIBUKA KIDEDEA KURA ZA MAONI CCM WILAYANI NKASI

DIWANI KATA YA KALA AFARIKI DUNIA KWA UGONJWA WA KIHARUSI

Mke wa Mchungaji wa kanisa la EAGT ajinyonga akihofia deni lake la fedha za kanisa