TASAC yaboresha kanuni kuongeza ufanisi



SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), limesikia kilio cha
wadau wa sekta ya usafiri kwa njia ya maji kwa kuboresha kanuni
mbalimbali ambazo zimekuwa ni kikwazo katika utendaji wao wa kila
siku.

Akizungumza kwa niaba ya wadau hao wa sekta ya usafiri kwa njia ya
maji, Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA),
Edward Urio amesema maboresho yaliyofanyika yamegusa maeneo
yaliyokuwa na utata mwingi katika utendaji wao.

Amesema upande wa mawakala wa forodha walikuwa na utata katika
ule muda wa kontena linaposhuka bandarini na linapofika kwenye
bandari kavu, ambako kulikuwa na upotevu wa siku mbili au tatu kwa
kuhoji jambo hilo lilipaswa kubebwa na nani jambo ambalo kanuni
hizo zimekuja na majibu yake.
“Lakini kuna suala moja kubwa kama unaagiza mzigo kwa kupitia
bandari hasa mzigo wa makasha, kuna utaratibu ambao unatakiwa
uweke dhamana ya kuweza kuaminiwa na wale mawakala wa meli
uweze kulichukua lile kisha ukapakue mzigo wako.

“Kama ni hapa Dar es Salaam, kama ni Morogoro, kama ni Arusha,
kama ni Malawi, Zambia, Congo, halafu ile dhamana ya lile kontena
inakuwa iko chini kwa wakala wa forodha mpaka litakapokuwa
limerudi kwenye sehemu yake husika ya kurudisha,” amesema.
Kwa maelezo yake gharama hiyo ilikuwa ni kubwa ambapo asilimia
kubwa ya wanachama wao ambao ni Watanzania walikuwa hawawezi
kuzimudu.

“Tulikuwa tunatakiwa kuweka takribani dola 3000 mpaka 5000
kwenye makasha ya futi 40 na dola 1000 mpaka 2000 kwenye
makasha ya futi 20. Unakuta kuwa ukiwa na kontena 10 ya futi 40
unatakiwa ulipe takriban dola  40,000,” amesema.

Amesema dola hizo 40,000 kwa wakala ambaye analipwa dola 200
kwa kila kontena ilikuwa ni maumivu makubwa.

Naye Mkurugenzi wa Udhibiti Huduma za Usafiri kwa njia ya maji
TASAC, Deogratias Mukasa amesema wamekutana na wadau wao
kutoa ufafanuzi kuhusu kanuni mpya nne ambazo zimepitishwa Juni
mwaka huu.

Amesema kanuni hizo zinahusu usalama wa mizigo, utendaji wa
shughuli ndani ya bandari na bandari kavu, usajli wa wasafirishaji
wanaouza na kusafirisha bidhaa kutoka Tanzania kwenda nchi za nje
kupitia bandari, pamoja na ya uhakiki shehena na ya uwakala wa
meli.

Amewataja wadau waliokutana nao ni bandari, bandari kavu,
mawakala wa meli, wagomboaji wa shehena, wakusanyaji na
watawanyaji shehena, wasafirishaji na mamlaka ya forodha.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Kaimu Mkeyenge amesema
shirika hilo linathamini utoaji elimu kabla ya kuanza utekelezaji wa
sheria au kanuni zake, na kwamba maboreesho ya kanuni hizo
yanalenga kuboresha utoaji huduma kwa usahihi na kuleta usawa
kwa wadau wote.

Comments

Popular posts from this blog

KAEGELE NA KAZUKAMWE WAIBUKA KIDEDEA KURA ZA MAONI CCM WILAYANI NKASI

DIWANI KATA YA KALA AFARIKI DUNIA KWA UGONJWA WA KIHARUSI

Mke wa Mchungaji wa kanisa la EAGT ajinyonga akihofia deni lake la fedha za kanisa