Masomo yaongezeka mtaala mpya msingi
TAASISI ya Elimu Tanzania imetoa mtaala wa elimu ya msingi kuanzia
darasa la kwanza hadi la saba 2023.
Muundo wa mtaala huo umebadilika na sasa elimu hiyo itakuwa ni ya
miaka sita badala ya saba kama ulivyokuwa Mtaala wa Elimu ya
Msingi wa mwaka 2016.
Mtaala huo umezingatia nadharia za ukuaji na ujifunzaji na falsafa ya
elimu ya kujitegemea inayosisitiza elimu inayomwezesha Mtanzania
ajitegemee na amudu maisha yake ya kila siku.
Muundo wa mtaala unaonesha elimu ya msingi itatolewa kwa miaka
sita katika hatua mbili ambazo ni darasa la kwanza na la pili ili
kujenga umahiri katika stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu
(KKK).
Katika hatua ya pili inaonesha mtaala huo utaanzia darasa la tatu hadi
la sita na italenga kuimarisha stadi za KKK na stadi nyingine za
maisha.
Mwanafunzi wa shule ya msingi anatakiwa aanze darasa la kwanza
akiwa na umri wa miaka sita na kumaliza darasa la sita akiwa na umri
wa miaka 11.
Kwa mujibu wa mtaala huo mwaka wa masomo utakuwa na siku 194
sawa na wiki 39 na umegawanyika katika mihula miwili inayolingana.
Katika kila muhula wiki mbili zitatumika kwa ajili ya upimaji endelevu
na tamati.
Vipindi na muda wa ufundishaji na ujifunzaji katika elimu ya msingi
utakuwa dakika 30 kwa kila kipindi kwa darasa la kwanza na la pili na
dakika 40 kila kipindi kwa darasa la tatu hadi la sita.
Katika eneo la Dira, Malengo na Umahiri wa Jumla, mtaala umelenga
kuwa na Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi na
mitazamo chanya, anayethamini usawa, haki na elimu bila ukomo
katika kuleta maendeleo endelevu ya kitaifa na kimataifa.
Kwa mujibu wa mtaala huo, maeneo ya kujifunza na umahiri mkuu
kwa darasa la kwanza na la pili yamezingatia ujenzi wa lugha,
mawasiliano na stadi za hisabati, utamaduni, sanaa, michezo na afya
na mazingira.
Kwa darasa la tatu hadi la sita maeneo ya kujifunza na masomo
yamezingatia kumjengea mwanafunzi umahiri wa lugha na
mawasiliano, hisabati, sayansi ya jamii, sayansi na teknolojia na sanaa
na michezo.
Katika eneo la lugha wanafunzi hao watajifunza masomo ya lugha za
Kiswahili, Kiingereza, Kichina, Kiarabu na Kifaransa.
Mtaala umeelekeza kuwa katika eneo la sayansi ya jamii watakuwa na
masomo ya historia ya Tanzania na maadili, Jiografia na mazingira,
hisabati, sayansi, sanaa na michezo.
Aidha, lugha ya kufundishia kwa mujibu wa mtaala huo Sera ya Elimu
na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023 inaelekeza
matumizi ya lugha ya Kiswahili, Kiingereza, Lugha ya Alama Tanzania
(LAT) na lugha nyingine za kigeni katika elimu na mafunzo.
Sera inatamka kuwa lugha ya Kiswahili itatumika kama lugha ya
kufundishia katika shule zinazotumia Kiswahili na Kiingereza
kitatumika katika shule zinazotumia Kiingereza kama lugha ya
kujifunzia na kufundishia.
Aidha, masomo ya lugha za Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, Kichina
na Kiarabu yatafundishwa kwa lugha inayohusika.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Elimu katika Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia, Dk Lyabwene Mtahabwa mtaala huo umeandaliwa kwa
kuzingatia Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka
2023.
Dk Mtahabwa pia alieleza kuwa mtaala umezingatia maoni ya wadau
yaliyokusanywa na kuchakatwa kati ya mwaka 2021 na mwaka jana
na matokeo ya uchambuzi wa maandiko kuhusu uzoefu kutoka nchi
nyingine.

Comments
Post a Comment