Walimu watakiwa kuutumia muda wa ziada kufanya shughuli zao za kiuchumi kujiongezea kipato


Na Israel Mwaisaka,Rukwa

MKUU wa wilaya ya Nkasi Peter Lijualikali amewataka Walimu kuutumia vizuri muda wao baada ya kazi kujishughulisha na shughuli nyingine za kiuchumi kama kilimo na ufugaji ili kuweza kujiongezea kipato.

Rai hiyo ameitoa jana kwenye ufunguzi wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) wilaya Nkasi ambapo alidai kuwa kimsingi mishahara haiwezi kutosheleza mahitaji yote ya kijamii na hivyo kujishirikisha katika shughuli nyingine za kiuchumi ili kukuza kipato chao.

Alisema kuwa wilaya Nkasi ni moja ya eneo zuri sana kwa kilimo na ufugaji na kuwa kama watajikita katika sekta hiyo ya kilimo na ufugaji ni rahisi san asana kuweza kujikwamua kiuchumi na kuweza kuifanya vyema kazi yao ya Ualimu na kuweza kuleta tija mahala pao pa pazi.

Pia aliwasihi Walimu kuendelea kulinda maadili ya kazi yao na kuwa kwa kufanya hivyo kutaifanya kazi yao kuheshimika na wao kuwa kioo katika jamii badala ya wao kuwa watu wa hovyo na kuwa kitu hicho hakikubaliki.



Awali katibu wa CWT wilaya Nkasi Mustafa Mitago alimweleza mkuu huyo wa wilaya kupitia risala yao kuwa bado wao kama walimu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hasa za madai ya fedha isiyo mishahara kama fedha za matibabu,likizo,Uhamisho na Kikokotoo licha ya serikali kufanya mabadiliko kadhaa kwenye kikokotoo hicho lakini wao wanahitaji kikokotoo cha zamani na kuwa hiki cha sasa bado kinawanyanyasa wastaafu.

Alisema kuwa kero hizi ndogondogo zinashusha molari kwa Walimu na kushindwa kufanya kazi kwa weredi mkubwa na kuwa wanaomba jkero hizo kutatuliwa kwa haraka ili mwalimu aweze kufanya kazi yake kwa weredi na tija ionekane

“” Ni vyema sasa kero hizi ndogo ndogo kutatuliwa kwa wakati kwani kuna wakati maendeleo ya kielimu yanakua siyo mazuri na hii inatokana na Walimu hawa kuendelea kufanya kazi kwa kinyongo kitu ambacho siyo kizuri””

Sambamba na hilo aliwataka Walimu kutekeleza wajibu wao sawasawa kwani hakuna haki bila wajibu na kuwa wao waendelee kutimiza wajibu sawasawa na wakati huo haki zao zinashughulikiwa.

Katika mkutano huo wa Uchaguzi Gidioni Ngorogoro alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa CWT ambapo alitetea nafasi yake kwa mara ya pili kwa kupata kura 133 na kukataliwa na kura 11,mweka hazina Seleman Nestoery ambaye pia alitetea nafasi yake kwa kupata kura 60 dhidi ya wapinzani Wake Watano waliogawana kura 83 na kumfanya mtunza hazina huyo kupenya katika nafasi hiyo.

Nafasi nyingine zilizopata viongozi ni Mwakilishi wa walimu Wanawake,Hiba Mariamu Abdalah,Mwaklilishi Walemavu Mfupe Noelia,Mwakilishi wa walimu vijana Sangu Liberatus,Wawakilishi shule za sekondari Francis Kang’ombe na Philbert Sadala,Wawakilishi shule za msingi Yonas Mahuvi,Mwalimu Nduva,Daniel Mpepo na Thomas Christopher .Mwakilishi shule za awali Stanley Fimbo,Mwakilishi wa taasisi na uongozi Thobias Mhagama.

Viongozi hao waliochaguliwa watadumu katika nafasi zao katika kipindi cha miaka mitano ijayo


Comments