WANANCHI KYELA WANG'AKA KWA MAMLAKA YA MJI MDOGO KUTAKA KUVUNJWA

                        

                   MAKALA

Na Ibrahim Yassin,

yassin,ibrahimu@yahoo.com 0718382817

IMEELEZWA kuwa siasa za hila,maji taka,chuki binafsi uelewa mdogo kwa baadhi ya viongozi wilayani Kyela mkoani Mbeya zatajwa kuwa ni chanzo cha kutaka mamlaka ya mji mdogo wa Kyela uvunjwe Dira kamilifu limebaini.

Mwandishi wa Dirakamilifu aliweka kambi ya siku 20 wilayani humo kuzungumza na wananchi pamoja na viongozi wa pande zote kutaka kujua mamlaka ilianzishwa kwa sababu ipi na nini sababu ya kutaka kuvunjwa.
Chief Kennedy Koroso Mwananchi na kiongozi mstaafu wa CCM anasema kwa upande wake haoni sababu ya uwepo wa mamlaka ya mji mdogo kwani imekaa zaidi ya miaka 10 imeshindwa kupata hadhi kuwa halmashauri ya mji kama ilivyo Tunduma.


Anasema wakati tunduma iliyopo mkoani Songwe imepaishwa kuwa mamlaka ya mji mwaka huo huo Kyela nayo ilipaishwa ,lakini Tunduma imepaishwa kuwa halmashauri ya mji katika kipindi cha miaka 3 pekee lakini Kyela ni zaidi ya miaka 10 haijapata hadhi hivyo alishauri ivunjwe.

Nae Herry Athuman kada lialia wa chama cha mapinduzi wilayani humo,anasema mamlaka ya mji mdogo iliwekwa kisiasa na imekaa muda mrefu pasipo kupaishwa kuwa halmashauri ya mji hivyo ni bora ifumuliwe irudi kwenye mfumo wa vijiji ili wajipange upya.

Josephat Longoli mwenyekiti mstaafu wa mamlaka ya mji huo aliyeuongoza toka 2014 hadi 2019 kupitia (Chadema) akipokezana na Karrison Bongo (CCM) ambaye walitoshana kura anasema kuna kila sababu mamlaka kuendelea kuwepo kutokana na faida iliyopo.

Anasema mamlaka ya mji mdogo Kyela iliombwa mwaka 2004 na kuanza kazi mwaka 2008 lengo ni kusogeza huduma karibu na wananchi,huku akisema mikutano ya kushirikisha wananchi vilikaliwa na baraza la madiwani lilipitisha.

Anasema katika kipindi cha miaka michache mamlaka imepiga hatua za maendeleo kwa kujenga barabara kwaTsh,zaidi ya Milioni 54,na makaravati 79,Vizimba vya taka,Shule za sekondari na msingi karibu kata zote 14 zilizopo ndani ya mamlaka ya mji mdogo.



Anasema vigezo vyote vya kuwa mamlaka ya mji mdogo vipo kwani kabla ya kupewa mamlaka kulikuwa na chuo kimoja,shule 1ya Itope sekondari,kituo 1 cha polisi,idadi ya maduka ya kuhudumia jamii 250 huku idadi ya watu ikiwa 60,000.

Anasema baada ya kupewa mamlaka waliongeza huduma za kijamii,shule zipo zaidi ya 8,hospitali 1 na vituo vya afya zaidi ya 3,maduka ya kutolea huduma kwa wananchi yapo zaidi ya 1,000 vyuo vipo 3 na idadi ya watu ni 2,21,490 kwa mujibu wa sense ya watu na makazi ya 2012.

Mbali na hilo pia anasema wameweza kutoa Tah,Milioni 23 kununua eneo la masiko,na katika mchango wa mwenge wa uhuru mamlaka ilichangia Tsh,Milioni 40,halmashauri ilichangia Milioni 28,hao wanaosema mamlaka inaendeshwa na halmashauri wamepotoka.

Anasema uelewa mdogo na miemko ya kisisa kwa baadhi ya watu wakiwemo viongozi wantaka mamlaka isiwepo wakidhani inalelewa na halmashauri ya wilaya kumbe si hivyo,kwani mamlaka ina bajeti yake na inavyanzo vya mapato inajiendesha yenyewe.

Naye Karrison Bongo mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Kyela anayeongoza hadi sasa,anasema kuna baadhi ya watu ama viongozi wanaendesha siasa za chuki,wamekosa hoja za msingi za kutaka mamlaka ivunjwe.

Bongo amesema mamlaka ya Mji mdogo ilianzishwa kisheria ambapo amesema sheria No;17 ibara ya 3 na sheria N0; 17 ibara ya 9 inaipa mamlaka ya mji mdogo kuwa na Nembo yake, Mhuri wake, kushtaki na kushakiwa kwa jina lake hivyo kufutwa nako kunatakiwa kufuate taratibu na sio ama ambavyo wanavyoongea mitaani.


Anasema uwepo wa mamlaka ya mji mdogo wao kama viongozi wakishirikiana na wenyeviti wa vitongoji na wataalam wameweza kukusanya fedha na kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kununua gari la kuzolea taka ngumu wametoa zaidi ya Milioni 100 kuchangia ununuzi wa gari la kuchongea barabara (SKAVETA).

Bongo anasema Mamlaka hiyo imeweza kujenga barabara ya Magereza kwenda Serengeti hadi Mbugani yenye urefu wa kilomita moja kwa gharama ya Tshs26.8 milion na barabara ya Community center au Mashimoni yenye urefu wa kilomita 0.4 kwa gharama ya Tshs41.5 million

Vile vile ameongeza kuwa Mamlaka hiyo imenunua eneo la kuzikia watu eneo la Itope kwa gharama ya Tshs20 milioni pia amesema wamejenga makaravati sita kwa gharama ya shillini million 43.8 pesa kutoka mapato ya ndani.

Aidha anasema kuwa kwa kutaja vichache kati ya vingi ambavyo mamlaka hiyo imevifanya ni pamoja na ujenzi wa zahanati ya Ndandalo kwa gharama ya Tshs60 milion, ununuzi wa eneo la kuweka taka ngumu kwa gharama ya Tshs20 milion.

Bongo anaesema kuwa inasikitisha kuona kuwa hata Mbunge anaunga mkono mamlaka kufutwa huku akijua kuwa huko nikurudisha nyuma maendeleo ya Wanakyela.

Mwenyekiti huyo alikumbushia pia kuwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri kipindi hicho Kipija pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya kipindi hicho Abdallah Kihato nao walijaribu kusitisha mchakato wa kuanzisha mamlaka hiyo kwa kile walichodai kuwa madiwani walifoji mitasali kwa kutowashirikisha wananchi jambo ambalo lilishindikana.

Anasema mtu ambaye alikuja kulimaliza suala hilo alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kipindi hicho John Livingston Mwakipesile ambaye aliunda tume ya uchunguzi ili kubaini ukweli wa jambo hilo lakini ukweli ukabaki kuwa hakukuwepo na kugushi kwa mitaasali kwa kuwa wananchi walishiriki kikamilifu kutaka mamlaka ianzishwe

Mwenyekiti mstaafu wa halmashauri ya wilaya ya Kyela Dr,Hunter Mwakifuna akizungumza kwa njia ya simu kuhusu sakata hili,anasema wanaotaka mamlaka ifumuliwe wanatakiwa kupewa elimu ili wajue faida na hasara zake.

Anasema mamlaka ilianzishwa kwa mujibu wa sheria ibara ya 146 ya katiba inayoonesha wazi uwepo wa kusogeza huduma kwa wananchi ,mikutano ilifanyika kushirikisha wananchi walielezwa faida na hasara za uwepo wa mamlaka na wananchi waliridhia na baraza lilipitisha kupitia vikao.

Anasema wakati mchakato wa kuanzisha mamlaka kulikuwa na vijiji 6 ambavyo vilimegwa kuwa vitongoji 40 zikazaliwa kata 14 kutoka kata moja ya Kyela,ambapo baraza la madiwani kwa wilaya nzima kata zipo 33,kata za CCM viti maalum jumla 41.

Anasema madiwani hao ni wengi kwa mkoa mzima Kyela inashika nafasi ya 3 kuwa na madiwani wengi,’’Tunaomba waandishi wa habari mtusaidie kutoa eliu uwepo faida ya mamlaka,watu nwaache kuzungumza mambo mepesi mepesi’’.

Dirakamilifu ilimtafuta Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kyela Kingamkono Katule ambaye anaongoza vikao vya mabaraza ya madiwani kutaka kujua iwapo anafahamu kuwa mamlaka hiyo wanataka ivunjwe.



Kingamkono anasema japo suala hilo analifahamu lakini kama kiongozi hawezi kulizungumzia zaidi ya kusema tunasubiri maamuzi ya TAMISEMI.

Mbunge wa jimbo la Kyela Ali Mlagila (Kinanasi ) alipopigiwa simu kuzungumzia sakata hili kwa mara kadhaa hakuonesha ushirikiano licha ya kuwa baadhi ya watu wanadai kuwa ni miongoni mwa viongozi wanaopendekeza kuvunjwa kwa mamlaka.

Akihitimisha juu ya sakata hilo Mkuu wa Wilaya ya Kwela Josephine Manase anasema anachokifahamu yeye ni kwamba Mamlaka bado inaendelea kuwepo kwa kuwa hakuna taarifa zozote kutoka Tamisemi iliyomYfikia kuhusu kufutwa kwa mamlaka ya Mji mdogo wa Kyela.

Mkuu huyo anasema hivi karibunu wamebata barua kutoka TAMISEMI ambayo ilikuwa inatoa miongozo ya uandikishaji wa daftari ya kupiga kura ambapo Mamlaka hiyo nayo imo hivyo taarifa za kufutwa sio za kweli.

Kutokana na kasi ya maendeleo ilivyo hivi sasa kwa wilaya ya Kyela ,ipo haja mamlaka ya mji mdogo ikapandishwa hazi na kuwa mamlaka ya mji na hatimaye kuwa halmashauri ya mji ili kusogeza huduma karibu na wananchi wanaotaka mamlaka ivunjwe wapuuzwe.

Comments